WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame, amekutana na wafanyabiashara wanaoingiza ng’ombe nchini kupitia bandari za KisaKasaka na Donge Muwanda, kwa lengo la kujadili kupanda kwa bei ya nyama na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika ukumbi wa ASSP Maruhubi, Waziri Makame alisema serikali imeamua kuwaita wadau hao ili kusikiliza maoni yao kuhusu mfumuko wa bei ya nyama, ambayo kwa sasa Inauzwa kati ya shilingi 19,000 hadi 20,000 kwa kilo moja.
Alisema ongezeko hilo limekuwa likilalamikiwa na wananchi wengi, hivyo serikali imeona umuhimu wa kukaa pamoja na wadau ili kubaini chanzo halisi cha tatizo na kuchukua hatua stahiki.
“Tumewaita wafanyabiashara hawa ili tusikilize changamoto zao na kupata suluhisho la pamoja litakalosaidia kudhibiti bei ya nyama”, alisema Waziri Makame.
Alibainisha kuwa serikali imepokea hoja mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara hao, na imepanga kuchukua hatua ikiwemo kuanzisha jumuiya ya waingizaji wa ng’ombe ili kuimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli zao.
Aidha, alisema serikali itaanza rasmi usajili wa wafanyabiashara wote wanaoingiza mifugo nchini, hatua itakayosaidia kujua idadi yao, maeneo wanayotumia kama KisaKasaka na Donge Muwanda pamoja na utaratibu wanaofuata katika biashara hiyo.
Aliongeza kuwa serikali itashirikiana na Halmashauri za Kaskazini ‘A’ na Kaskazini ‘B’ pamoja na taasisi husika, ikiwemo Wizara ya Mifugo ya Tanzania Bara, kupitia upya mfumo wa tozo ili kuhakikisha unakuwa rafiki kwa wafanyabiashara bila kuathiri mapato ya serikali.
“Ni muhimu kuweka uwiano wa tozo hizi ili kuepusha mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara ambao hatimaye huathiri bei kwa wananchi,” alisisitiza.
Kwa upande wao, wafanyabiashara walieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto ya uwepo wa tozo nyingi kutoka pande zote za Zanzibar na Tanzania Bara, hali inayoongeza gharama za uingizaji wa mifugo.
Pia walishauri kuwepo kwa mfumo bora wa usimamizi pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya machinjio, ili kurahisisha shughuli za biashara na kupunguza gharama zisizo za lazima.
