NA KHAMISUU ABDALLAH
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema Tanzania inaendelea na utaratibu wa kuwarejesha raia wake waliokwama nchini Dubai kutokana na vita vinavyoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili, Hamza Hassan Juma, aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Vuga Mjini Unguja.
Alisema waziri wa Mambo ya Nje wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mahmoud Thabit Kombo, tayari ameshatoa maelekezo kwa ubalozi ambao anashughulikia ukusanyaji taarifa za abiria waliokwenda Dubai kwa mashirika ya ndege mengine ili kufanyiwa taratibu za kuwarudisha Zanzibar.
Alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar imeanza kufanya jitihada za kutafuta namna ya kuwarudisha raia wa Tanzania ambao wamekwama nchini Dubai waliosafiri na mashirika mengine ya ndege.
“Wapo wananchi wa Zanzibar wanaosafiri kupitia mashirika mengine ya ndege ambao wamekwama nchini humo waliokwenda kwa ajili ya shughuli za kibiashara ukizingatia Dubai ni kitovu cha biashara”, alisema.
Alieleza kwamba zaidi ya watu 40 wamekwama Dubai katika shughuli zao za kibiashara wameishiwa na pesa, wengine wameanza kuhama hoteli na wanaishi katika sehemu za miskiti na maeneo mengine.
“Asubuhi nimekaa na Makamu wa Pili na kuniuliza hatua tuliyofikia na tayari ubalozi wa Tanzania uliopo Dubai umeshaanza kupeleka orodha ya majina na wakishatimia idadi tunayoitaka serikali itatuma ndege kwa ajili ya kuwarudisha nchini,” alisema.
Hivyo, aliwaomba wananchi ambao wana ndugu zao kuwa na subira huku serikali ikifanya utaratibu wa kuwarudisha nyumbani ndani ya siku mbili ili waendelee kuungana nao.
Hata hivyo, alisema tayari Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ilipeleka ndege kwa ajili ya kuchukua abiria ambao walisafiri na Air Tanzania ambao walikwama nchini humo takriban 235 tayari wamesharudi nchini.
Waziri Hamza aliwasisitiza wananchi wa Zanzibar hasa vijana kulinda tunu ya amani kwani machafuko hayo ni funzo kwao kuhakikisha wanalinda lulu hiyo waliojaaliwa na Mwenyezimungu.
“Vijana wafahamu kuwa ushabiki ni jambo moja lakini uhalisia ni jambo jengine wasipende kushabikia mambo ambayo hayatusaidii kwani vurugu zinawafaidisha watu wengine na sio sisi tulio huku, hivyo tulindeni tunu ya amani tuliyonayo,” alisema.
Aliwasisitiza kuendelea kupendana na kushirikiana kwani amani na utulivu ni jambo la msingi kwa uhai wa mtu na nchi kwa ujumla.
