Skip to content

Serikali kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria na Utawala Bora Dk. Haroun Ali Suleiman, amesema mwaka huu wa fedha serikali itaongeza viwango vya mishahara ya watumishi wa umma ili kuimarisha mazingira ya kiutendaji.

Aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya wizara hiyo katika siku 100 za uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Rahaleo.

Alisema kuwa serikali katika nyongeza hiyo itawatizama zaidi watumishi wanaopokea mishahara ya kiwango cha chini kwa dhamira ya kuwanyanyua kimaslahi.

Dk. Haroun alisema kuwa serikali ya awamu ya nane haina changamoto ya uhaba wa fedha kutokana na kuimarisha mifumo imara ya uthibiti wa fedha sambamba na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma.

“Mapato yamepanda na kufikia bajeti ya mwaka huu wastani wa trilioni 8 hivyo wafanyakazi wakati wowote kaeni mkao wa kula”, alisema

Aidha Waziri Dk. Haroun aliwataka watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na kuheshimu sheria na misingi ya utumishi ya umma hasa ikizingatiwa serikali imekuwa ikiwapatia haki na stahiki zao kikamilifu.

Akizungumzia kuhusu upandishwaji wa madaraja kwa wafanyakazi alisema utaratibu huo utasaidia kuwamsha watendaji wavivu, wazembe na wenye kuendelea kufanya kazi kwa mazoea badala ya kuona miongoni mwao wanapata nyongeza ya mshahara kufuatia uwajibikaji bora.

“Utaratibu huu umelenga kuongeza hamasa na bidii na uwajibikaji mzuri kwa watendaji kwani katika taasisi zetu wapo baadhi ya wafanyakazi hawawajibiki vyema na mara nyingi hufurahia pale zinapokuja nyongeza kwa watu wote”, alisema.

Aliwasisitiza viongozi wa taasisi kuhakikisha wanasimamia vizuri suala la kuwapima wafanyakazi wao kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ili kila mmoja aweze kupata stahiki yake.

Alifahamisha kwamba kiongozi wakati mwengine hulazimika kumwajibisha mfanyakazi kwa lengo la kumjenga kiutendaji pale anapokwenda kinyume na taratibu za utumishi.

“Wapo viongozi humuwajibisha mtumishi kwa nia njema tu ikiwemo kumfundisha misingi ya kuheshimu maadili ya kazi lakini viongozi wengine humuadhibu mtumishi kwa kumkomoa tu”, alieleza.

Hata hivyo alisema serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya unyanyasaji wa watumishi ikiwemo kupangiwa majukumu kinyume na taaluma yake.

Dk. Haroun aliwaomba viongozi wa taasisi kuhakikisha kila mtumishi anafanyakazi kulingana na taaluma alionayo kwani itasaidia kuleta ufanisi na mageuzi ya kiutendaji.

Katika hatua nyengine alisema ndani ya siku 100 wizara imefanikiwa kufanya uchambuzi wa maposho nà kupanua wigo wa ulipaji wa posho la wakuu wa divisheni katika wizara na taasisi ambapo awali lilikuwa likilipwa kwa Idara za Mipango, Sera na Utafiti pamoja na Idara ya uendeshaji na utumishi tu. 

Alisema hatua hiyo ipo sambamba na kuimarisha matumizi ya miundo ya utumishi ambapo hivi sasa inatumika kwa ufanisi katika kupandisha vyeo, madaraja na marekebisho ya mishahara kuanzia Julai 2022.