Skip to content

Serikali kukabiliana na changamoto bandarini

  • Zanzibar

NA ASYA HASSAN

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ina kazi kubwa ya kufanya ili kuondosha changamoto zinazoikabili Bandari ya Malindi, ambayo kwa sasa imekuwa ikikabiliwa na msongamano mkubwa wa abiria na mizigo.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Badria Atai Masoud, alisema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa vyombo vya usafiri wa baharini.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi za serikali pamoja na wawakilishi wa makampuni ya usafiri wa baharini.

Alisema bandari ya Malindi ni ndogo kwa kuwa ilijengwa miaka mingi iliyopita, katika kipindi ambacho mahitaji ya huduma za usafiri hayakuwa makubwa kama yalivyo sasa.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Shirika la Bandari Zanzibar, PC Ussi Mshimba Mbarouk, alisema Bandari ya Malindi kwa sasa haikidhi mahitaji ya utoaji wa huduma.

Mapema akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Mtumwa Said Sandal, alisema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau katika kutatua changamoto za usafiri wa baharini.