Skip to content

Serikali kujenga jengo jipya la Baraza la Wawakilishi

Serikali inatarajia kutumia shilingi bilioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa jengo la Baraza jipya la Wawakilishi pamoja na ulipaji wa fidia kwa wakaazi 421 wa Ziwa Maboga.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, aliyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa mafanikio ya siku 100 ya kipindi cha pili cha uongozi wa Dk. Mwinyi.

Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 21 zitatumika kwa ujenzi wa Baraza la Wawakilishi la kisasa katika eneo la Kisakasaka na shilingi bilioni nane kwa ajili ya ulipaji wa fidia za wananchi watakaopisha ujenzi wa nyumba za kisasa katika maeneo hatarishi ya Ziwa Maboga.

“Tumeshaanza taratibu za ujenzi wa mradi wa Baraza jipya la Wawakilishi utaozingatia vigezo, ubora na mahitaji ya sasa na baadae na tutajenga nyumba za kukodisha wajumbe”, alisema.

Sambamba na hilo, waziri Hamza alisema serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi imeamua kufuatilia maeneo yote hatarishi ili kuthibiti majanga na maafa hasa kipindi cha mvua zinazonyesha nchini.

“Tumenunua ‘drone’ moja na hivi karibuni tutaongeza nyengine kwa ajili ya utambuzi wa idadi ya maeneo hatarishi na kufanya uchunguzi wa tafiti mbalimbali za kimazingira”, alisema Hamza.

Alifahamisha kwamba katika hatua ya awali wizara imebaini maeneo 30 ambayo yapo katika mazingira hatarishi na serikali ipo katika mchakato ya kuleta suluhisho la kudumu.

Alitaja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa mitaro ya kupitishia maji ya mvua na misingi ya maji machafu.

Hata hivyo, Waziri Hamza aliwaomba masheha kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na utamaduni wa kujenga maeneo hatarishi pamoja na kununua maeneo yenye asili ya kujaa kwa maji ili kuepuka majanga.    

Kuhusu ulipaji wa fidia alisema kuwa tayari serikali imeshaanza kufanya tathmini katika eneo hilo na kueleza kwamba wakati wowote wananchi watapatiwa fedha na kutakiwa kuondoka katika eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu eneo la Ziwa Maboga, waziri Hamza alisema kuwa serikali inatarajia kujenga bwawa la kisasa ili kuondosha usumbufu wa kutuama maji katika eneo hilo

Alisema jumla ya nyumba 421 za makaazi katika eneo la Ziwa Maboga zimefanyiwa tathmini ili kupisha na ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara baada ya wananchi kupewa fidia zao.