Skip to content

Serikali kujenga hospitali mbili kubwa za rufaa – Dk. Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa serikali inakusudia kujenga hospitali nyengine mbili kubwa za rufaa zitakazotoa huduma za kisasa za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo ikulu mjini Zanzibar kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kampuni ya Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Limited ya nchini China.

Alizitaja hospitali mbili mpya zitakazojengwa kuwa ni hospitali ya Matibabu ya Magonjwa ya Saratani, Moyo na Mifupa na hospitali ya Rufaa na Kufundishia Watendaji wa Sekta ya Afya, itakayojengwa Binguni.

Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mngereza Miraji Mzee, alisaini kwa niaba ya serikali ya Zanzibar, huku Mkurugenzi wa Kampuni ya Jiangxi International, Peng Chao, akisaini kwa niaba ya kampuni hiyo.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Dk. Mwinyi alieleza kuwa tukio hilo ni ishara ya dhamira ya serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Alisema kwamba ujenzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja utakwenda kubadilisha hospitali hiyo na kuwa mpya yenye hadhi ya kisasa.

Aidha, alibainisha kuwa sekta ya afya ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, kwani wananchi wenye afya bora ndio msingi wa ujenzi wa uchumi imara na uimarishaji wa utoaji wa huduma bora na za kisasa.

Alisema kuwa baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali kuanzia ngazi ya msingi, wilaya na mkoa, hatua inayofuata ni kujenga hospitali tano katika kila mkoa, zitakazotoa huduma za kisasa zenye viwango vya kimataifa na kuendeshwa kitaalamu.

Alieleza kuwa kukamilika kwa hospitali hizo kutaiwezesha Zanzibar kuondokana na utaratibu wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, kwani huduma za matibabu ya kibingwa zitapatikana nchini kwa ubora na viwango vinavyokubalika kimataifa.

Alisema hospitali ya Mnazi Mmoja, inaandika historia mpya na kuipongeza wizara ya Afya pamoja na watendaji wote waliofanikisha kukamilika kwa mkataba wa mradi huo.

Aidha, aliipongeza Wizara hiyo kusimamia kwa karibu kampuni ya ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa.

Mradi wa ujenzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja unatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya BADEA, Kuwait Fund na Saudi Fund, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2027.