WIZARA ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo wakiwemo Shirika la CDC na AMREF Health Africa Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, hususani utoaji wa huduma za methadone kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza katika hafla maalum, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mngereza Mzee Miraji, aliishukuru AMREF na CDC kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha huduma za afya kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi kiafya.
Alieleza kuwa licha ya Zanzibar kuwa na kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kilicho chini ya asilimia moja kwa jamii kwa ujumla, bado changamoto ipo kwa watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya sindano, ambapo kiwango cha maambukizi kinafikia asilimia 9.3.
Dk. Mngereza alisema huduma za tiba mbadala ya utegemezi wa dawa za kulevya (MAT) zimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza madhara ya matumizi ya dawa hizo, kuzuia maambukizi mapya ya VVU pamoja na kusaidia waathirika kurejea katika maisha ya kawaida.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha miaka kumi ya ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, CDC na AMREF, zaidi ya familia 1,800 zimefikiwa na huduma hizo, huku takribani watu 300 wakirejea na kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa AMREF Tanzania, Dk. Florence Temu, alisema hadi kufikia Disemba mwaka jana jumla ya watu 1,831 walikuwa wamepatiwa huduma za OAT/MAT kupitia programu hiyo.
Alibainisha kuwa huduma hizo zinajumuisha upimaji na matibabu ya VVU, uchunguzi na tiba ya kifua kikuu, huduma za homa ya ini pamoja na ushauri nasaha na elimu ya afya.
Aidha, wahudumu 21 wa afya na waelimishaji rika wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu, huku watumishi watatu wa mradi huo wakitarajiwa kuajiriwa na Serikali ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi na endelevu.
