Skip to content

Serikali kufidia gharama bei ya mafuta

  • Blog

NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema itaendelea kuchukua hatua za kufidia gharama za bei ya nishati ya mafuta ikiwa bidhaa itapanda katika soko la dunia ili kupunguza athari kwa wananchi kuhakikisha wanaendelea kumudu gharama za maisha.

Waziri wa Maji Nishati na Madini, Nadir Abdullatif Alwardy aliyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari nje ya ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege.

Alisema serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mabadiliko ya bei yanayotokea katika soko la kimataifa hayaathiri kwa kiwango kikubwa watumiaji wa nishati nchini, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo vita vinavyoathiri uchumi wa dunia.

Alisema kupanda kwa bei ya nishati hakutokani na sera za kodi za ndani ya Zanzibar, bali kunachangiwa zaidi na mabadiliko ya bei katika masoko ya kimataifa ambako bidhaa hizo zinakotoka.

“Bei inaweza kupanda kutokana na hali ya soko la dunia, hususan kutokana na migogoro na vita vinavyoendelea katika baadhi ya mataifa ya nghuba, hata hivyo, sisi hatupandishi kodi zetu kinachoweza kupanda ni kile cha soko la kimataifa, na pale bei zinaposhuka huko zinapotoka, basi hata huku kwetu pia hupungua”, alisema Nadir.

Aidha alisisitiza kuwa endapo bei ya nishati katika soko la dunia itaongezeka kwa kiwango kikubwa, hata kufikia mara dufu, serikali ipo tayari kuingilia kati kwa kutoa ruzuku au fidia ili kupunguza mzigo kwa wananchi akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kulinda ustawi wa wananchi pamoja na kuhakikisha shughuli za kiuchumi haziathiriki.

Hata hivyo alisema licha ya changamoto za soko la kimataifa, Zanzibar bado inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye bei nafuu ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki hali inayotokana na juhudi za serikali kusimamia sera na mifumo ya uagizaji na usambazaji wa nishati hiyo kwa ufanisi.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za nishati katika soko la dunia ili kuchukua hatua kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa gharama nafuu kadiri inavyowezekana.

Alisema tayari serikali imeshapata mafuta ya kuweka akiba hadi mwezi Juni mpaka Julai kutoka na changamoto ya vita iliyopo mashariki ya kati.

Naye mdau wa sekta ya anga Nassor Rajab alisema hali ya mafuta kimataifa ni lazima kukubali kwamba bei itapanda kutokana na mtikisiko wa vita kati ya Iran, Ukraine na Marekani hivyo lazima wananchi kujitayarisha kuendana na hali itakavyokuwa.

Aliziomba taasisi zinatoa huduma za mafuta ikiwemo ya ndege kuhakikisha mafuta yanapatikana na watalii waweze kuja nchini kwani viongozi wamefanya kazi kubwa kuhakikisha Tanzania inaendelea kukuza uchumi wake kupitia sekta hiyo.

“Zanzibar hivi sasa hakuna msimu ambao watalii hawaji ukilinganisha na miaka iliyopita hivyo ni lazima kila mtu kwa nafasi yake kuhakikisha kwamba anawajibika kama inavyotakiwa”, alisisitiza Nassor.