JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema serikali inafikiria kupeleka jeshi kwenye maeneo yenye ghasia za magenge ili kukabiliana na uhalifu unaohusiana na magenge hayo.
Matamshi ya rais yamejiri huku kukiwa na ongezeko la visa vya vifo vinavyohusiana na magenge katika maeneo kadhaa ya nchi.
“Wito umetolewa kupeleka jeshi,” Ramaphosa aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi asubuhi nje ya jengo la Lekgotla ya Kamati Kuu ya African National Congress, ambapo ni sehemu maalumu panapofanyika mikutano muhimu ya kisiasa au serikali.
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa askari wamepewa mafunzo ya kuzuia vitisho badala ya kufanya uchunguzi, hivyo uamuzi wowote wa kuwapeleka unahitaji kuzingatiwa kwa makini. Ramaphosa alisisitiza haja ya kuwa na njia yenye uwiano katika kushughulikia mzozo huo.
“Vurugu za magenge ni mojawapo ya changamoto ambazo tunakabiliana nazo. Hilo ni muhimu sana katika akili zetu,” Ramaphosa alisema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, takriban watu 26 waliuawa katika mfululizo wa ghasia zinazohusiana na magenge katika Cape Flats, Cape Town, Mkoa wa Cape Magharibi. Ghasia hizo zilijumuisha ufyatulianaji wa risasi katika Marikana, Mi mdogo wa Philippi Mashariki, ambao ulisababisha vifo vya watu wanane.
