Na Saida Issa, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,sayansi na Teknolojia imeanza maandalizi ya kuwasafirisha wanafunzi 34 waliomaliza kidato cha sita kwenda nchini Ireland kwa masomo ya sayansi na teknolojia, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan mbele ya Bunge.
Akizungumza jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya utekelezaji wa siku 100 za uongozi wa Rais Samia, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema wanafunzi hao walipatikana baada ya kufanya vizuri katika masomo ya hesabu na sayansi.
Alieleza kuwa lengo la kuwapeleka wanafunzi hao nje ya nchi ni kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika nyanja za teknolojia na ubunifu, akibainisha kuwa Ireland ni miongoni mwa nchi vinara duniani katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Profesa Mkenda alisema maandalizi yote muhimu tayari yamekamilika na ada za masomo kwa wanafunzi hao zinatarajiwa kulipwa mwezi Machi mwaka huu.
“Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwaandaa vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijiti na ni utekelezaji wa moja kwa moja wa ahadi ya Rais Dk. Samia,
Katika eneo la elimu ya juu, Profesa Mkenda alisema Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ili kupanua wigo wa wanufaika,”alisema.
Alisema katika mwaka wa fedha unaokuja, Serikali inalenga kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu hadi kufikia shilingi trilioni 1.2, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vya kifedha kwa wanafunzi wanaohitaji msaada huo.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo linaendana na maono ya Rais Samia ya kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata fursa ya kujiendeleza kielimu.
Aidha, Waziri huyo alisema walimu, wakufunzi pamoja na walimu tarajali 1,055 kutoka Halmashauri 104 nchini wamenufaika na vifaa vya kidijiti na saidizi vilivyogharimu shilingi bilioni 5.4, vilivyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, hususan kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“vifaa vilivyonunuliwa ni pamoja na kompyuta mpakato 680, vifaa tisa vya Brain Note Touch Pass, voice recorder 377, tablets 196 kwa walimu wanaotumia lugha ya alama, mashine 30 za Perkins Braille, vifaa 101 vya kusaidia kusikia pamoja na mashine za Everest Drill Embosser,”alisema.
Alisema mashine za Everest Drill Embosser zina uwezo wa kuchapisha maandishi ya nukta nundu (Braille) na maandishi ya kawaida, hivyo kuwawezesha walimu wasioona kufundisha kwa ufanisi na kuimarisha ujumuishaji wa wanafunzi wote darasani.
Prof.Mkenda alisema mpango huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum hawabaguliwi na wanapata haki sawa ya elimu kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita.
Vilevile, alisema utekelezaji wa ahadi za Rais Samia unaendelea sambamba na upanuzi wa fursa za elimu ya juu kupitia utoaji wa mikopo na ujenzi wa miundombinu mipya, ikiwemo ujenzi wa kampasi 16 mpya za vyuo vikuu katika mikoa ambayo awali haikuwa na kampasi hizo.
