NA SAIDA ISSA, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. Samia Suluhu Hassan, amefungua jengo jipya la makao makuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Ngome), lililojengwa katika eneo la Kikombo, jijini Dodoma, akisisitiza kuwa miundombinu hiyo inapaswa kutumika kuimarisha ufanisi wa ulinzi wa nchi na si kuwa alama ya fahari pekee.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisema mabadiliko ya haraka ya mazingira ya kimataifa yanahitaji taasisi za ulinzi kwenda sambamba na wakati, kwa kuzingatia mikakati thabiti na matumizi bora ya rasilimali.
Alieleza kuwa mafanikio yote ya maendeleo yaliyopatikana nchini yamejengwa juu ya msingi wa amani na utulivu, akionya kuwa bila ulinzi imara, jitihada za kuinua ustawi wa wananchi haziwezi kufanikiwa.
Aidha aliahidi kuwa serikali itahakikisha awamu mbili zilizosalia za mradi huo zinakamilika kwa wakati, ili kutimiza azma ya kuwa na makao makuu ya kudumu na ya kisasa ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Aidha, alikumbusha kuwa thamani ya jeshi haipimwi kwa majengo au vifaa pekee, bali kwa uzalendo na moyo wa kujitoa wa wanajeshi wake.
Aliwataka maofisa na askari kuendelea kuheshimu kiapo chao cha kazi, kulinda heshima ya jeshi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuchafua taswira ya taasisi hiyo mbele ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali, Jacob John Mkunda, alisema mradi huo umetokana na juhudi za kikosi kazi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kilichotekeleza ujenzi kwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama.

Alibainisha kuwa gharama za jengo kuu, ofisi na samani zake ni shilingi bilioni 121.
Alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo mwaka 1964, halijawahi kuwa na makao makuu ya kudumu na ya kisasa kama hayo, akisema uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa ukurasa mpya katika historia ya JWTZ.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, alisema jengo hilo limejengwa kwa kuzingatia dhana ya ulinzi wa kisasa, likiwa na mifumo itakayowezesha kuhifadhi na kusimamia rasilimali muhimu za usalama wa taifa na kuimarisha ulinzi wa taasisi ya urais dhidi ya changamoto za sasa na zijazo.
Katibu Mkuu wizara hiyo, Dk. Faraji Mnyepe, alielezea safari ya miaka 48 ya ujenzi wa ngome hiyo ya ulinzi, huku akisema gharama za ujenzi wa awamu zote ni shilingi bilioni 318.
Alisema awamu ya kwanza ni shilingi bilioni 121, awamu ya pili shilingi 107 bilioni na awamu ya tatu shilingi 90 bilioni.
Alisema wazo la kuunganisha Wizara ya Ulinzi, JKT na Makao Makuu ya Jeshi (Ngome) katika jengo moja lilianza miongo kadhaa iliyopopita lakini lilikwama kutokana na changamoto za kiuchumi.
Alisema mpango wa awali wa kujenga makao makuu ya awali ulianza mwaka 1970 ukiwa na lengo la kuimarisha uratibu wa taasisi hizo mbili pamoja na makao makuu ya jeshi, maarufu Ngome.
