NA MASANJA MABULA, PEMBA
WATU 40 wanaosadikiwa kuwa ni raia wa Congo wameokolewa katika bahari Yalikoni Kengeja wilaya ya Mkoani, baada ya chombo chao kuzama, huku watu wawili wakithibitishwa kufariki dunia katika ajali hiyo ya kusikitisha ya majini.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Miza Hassan Faki, alisema juhudi za uokoaji zilichukuliwa mara moja baada ya kupokea taarifa za kuzama kwa chombo hicho.
Alisema vikosi vya uokoaji kwa kushirikiana na wananchi vilifika haraka katika eneo la tukio na kufanikisha kuwaokoa manusura 40 wakiwa hai.
“Tulipokea taarifa mapema na mara moja tukaanzisha operesheni ya uokoaji. Tunashukuru juhudi hizo zimefanikisha kuokoa watu wengi, ingawa kwa masikitiko makubwa tumempoteza mmoja”, alisema.
Majeruhi hao walikimbizwa katika hospitali ya Abdalla Mzee kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa kwa taratibu zaidi.
Daktari dhamana wa hospitali hiyo, Dk. Aboud Khamis Maabad, alithibitisha kupokea majeruhi hao, wakiwa katika hali tofauti kiafya na baada ya kupokelewa waliingizwa moja kwa moja katika huduma za dharura.
“Tuliwapokea majeruhi wote pamoja na mwili wa marehemu na mara moja tukaanza kuwapatia huduma za haraka kulingana na hali ya kila mmoja. Kwa sasa hali za wengi wao zinaendelea vizuri”, alisema Dk. Maabad.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, aliushukuru uongozi wa hospitali ya Abdalla Mzee na wadau mbalimbali kwa juhudi zao katika kuwahudumia majeruhi hao.
“Nawapongeza madaktari, wauguzi na wote waliohusika katika zoezi hili kwa kujitoa kwao. Ushirikiano huu umeonesha dhamira ya dhati ya kuokoa maisha ya wananchi,” alisema.
Aliwataka wasafirishaji wa vyombo vya majini na wananchi kwa ujumla kuzingatia masharti ya usalama kabla ya kuanza safari ili kuepusha ajali kama hizo.
Aidha vyanzo vyengine vya habari zimeeleza kuwa maofisa Idara ya Uhamiaji walifika katika eneo hilo na ndipo walipothibitisha kuwa majeruhi hao ni raia wa Congo, ambapo walifikwa na mkasa huo wakielekea Comoro kwenda kutafuta maisha na kukimbia vita vinavyoendelea nchini kwao.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba mawakala wawili raia wa Comoro waliokuwa wakiwasafirisha kwa boti walitofautiana ndio wakakata kambo ya boti walioyokuwa wakisafiria na kuwaacha baharini bila ya kuwa na huduma cha chakula wala maji kwa siku 15.
Katika muda huo wale walioshindwa kuhimili safari na kufariki walilazimika kuwatosa baharini mbapo idadi yao haikufahamika.
