PEMBE ya Afrika ni eneo ambalo kwa mataifa ya ghuba yamegeuzwa kuwa uwanja muhimu wa mapambano kwa ushindani wa kikanda na kiuchumi, na linaonesha wazi jinsi wafalme wa mataifa ya ghuba wanavyopigania ushawishi wao.
Pembe hiyo inazijumuisha nchi za Ethiopia, Somalia, Djibouti na Eritrea, ambapo mtaalamu wa eneo la ghuba, Anna Jacobs alisema Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umekosolewa zaidi kutokana na uwepo wake mkubwa mashariki mwa Afrika.
UAE, imekuwa ikikosolewa sana kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa Sudan wa RSF ambao wamekuwa kipambana na jeshi la serikali ya Sudan linaloongoza nchi hiyo, hata hivyo UAE imekuwa ikikanusha madai hayo.
UAE pia iliikasirisha Somalia kutokana na kuwekeza Somaliland, jimbo lililojitenga la Somalia ambapo kampuni kubwa ya usafirishaji ya DP World imewekeza mamilioni ya dola katika kujenga bandari na uwanja wa ndege.
Wachambuzi na watalaamu wengi wanaiona UAE kuwa nyuma ya uamuzi wa Israel kuwa nchi ya kwanza kutangaza rasmi kuitambua Somaliland, kama taifa huru, tangu mwezi Disemba mwaka jana.
Jacobs anasema ni hatua ya kawaida yenye hatari kubwa inayofanywa na utawala wa Emirati kuunda upya mpangilio wa mifumo ya kikanda. Lakini vitendo kama hivyo vinaongeza mivutano na Saudi Arabia, mshirika wa UAE aliyegeuka kuwa adui.
Nchi hizo mbili za kifalme ziliungana mwaka 2014 kupambana na waasi wa Kihouthi nchini Yemen, lakini muungano huo umevunjika na sasa wanaviunga mkono vikosi pinzani nchini humo.
Kulingana na Jacobs, kijadi Saudia ililenga kuziunga mkono taasisi za serikali na hali iliyopo, lakini sasa iko kwenye mashambulizi dhidi ya UAE, ikiwa ni pamoja na Pembe ya Afrika. Ushindani wao unaunda ushirikiano mpya.
Kuna uvumi wa kuwepo makubaliano ya kijeshi yanayofanyiwa kazi kati ya Saudi Arabia, Misri na Somalia kwa lengo la kukabiliana na ushawishi wa UAE. Mwezi uliopita, Somalia iliyafuta makubaliano yote yaliyokuwepo kati yake na UAE.
Ethiopia ni nchi ya pili yenye watu wengi zaidi Afrika ikiwa na watu wapatao milioni 130, na pia inavutwa kuingia katika ushindani uliopo.
UAE ilimpatia Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed mkopo wa dola bilioni 33, muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka 2018 na nchi hizo zilikubaliana kubadilishana sarafu ya takribani dola milioni 800.
Kwenye kilima kinachoelekea mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kasri jipya linajengwa kwa ufadhili wa UAE.
Cameron Hudson, aliyekuwa mchambuzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba kiwango cha uwekezaji wa UAE nchini Ethiopia, kinachooneshwa katika kasri hilo la mabilioni ya dola, ni kikubwa sana kiasi kwamba kimeigeuza Ethiopia kuwa kibaraka.
Mnamo mwezi Disemba mwaka jana jeshi la Sudan liliishutumu Ethiopia kwa kuandaa mafunzo kwa ajili ya wanamgambo wa RSF ambao ni maadui wake.
Hali hiyo inaashirikia kuwa mafunzo yalifadhiliwa na UAE. Maofisa wa Ethiopia hawakujibu madai hayo walipoombwa na AFP kufanya hivyo. Pesa zinazotolewa kwa wingi na mataifa ya ghuba zinazidisha misuguano iliyopo katika eneo lote la Pembe ya Afrika.
Biraanu Gammachu, mtafiti wa Ethiopia alisema nchi zenye utajiri mkubwa za ghuba zina ushawishi wa hatari kwa nchi masikini, na zilizokumbwa na mizozo za Afrika Mashariki.
Gammachu alibainisha kuwa ni uhusiano usio na ulinganifu kati ya nchi zinazoibuka zenye nguvu ya kati na mataifa yanayotegemea wafadhili.
Alifafanua kuwa ushawishi wa nchi za Ghuba katika Bahari ya Shamu unaendeleza ukosefu wa utulvu katika ukanda huo.
Hali ya kutokuelewana kati ya Ethiopia na mpinzani wake wa muda mrefu, Eritrea imekuwa ikiongezeka, huku hatua ya kukamilika kwa ujenzi wa bwawa kubwa la umeme la Ethiopia katika Mto Nile ikiwa imeikasirisha Misri.
Matokeo yake ni kwamba Misri na Eritrea zimetafuta uhusiano wa karibu zaidi kati yao na Saudi Arabia ili kukabiliana na Ethiopia.
Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki ambaye husafiri mara chache, aliizuru Saudia mara mbili mwaka 2025, na hivi karibuni aliikosoa UAE kuhusika katika kuvuruga utulivu wa Sudan.
Hudson alionya kuwa Eritrea inaweza kujihusisha moja kwa moja katika vita vya Sudan na hilo linaweza kuzidisha mzozo wa kikanda.
