Skip to content

Operesheni ya ZRA yabaini ukwepaji kodi

  • Zanzibar

NA HAFSA GOLO

MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA), imetoa siku tatu kwa wafanyabiashara wanaokwenda kinyume na matumizi ya mashine za kielektroniki wakiwemo wanaodai mashine zao mbovu na waliokuwa bado hawajajisali.

Kamishna wa Kodi za ndani ZRA, Ali Adinan, alieleza hayo wakati wa ziara ya kuangaliwa uwajibikaji wa wafanyabiashara katika maduka ya Darajani SOUK.

Alisema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya ZRA kubaini wapo baadhi ya wafanyabiashara utoaji wa risiti haupo sawa na wengine wahajajisajili kabisa.

Aidha, alisema baadhi ya wafanyabiashara ambao hawajajisajili au kutotoa risiti kama inavyotakiwa ndani ya siku tatu basi hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kupatiwa adhabu ya kutozwa faini.

“Sheria kwa mtu asietoa risiti inamtaka kwa kila risiti moja alipe shilingi milioni mbili na mpokeaji ambae hajadai risiti yeye inamtaka kulipa shilingi 30,000,” alisema.

Kamishna Adinan alisema kwa sasa ZRA inatilia mkazo zaidi kwa wafanyabiashara wasiotoa risiti kwa hatua ya awali kuwapatia onyo lakini ikiwa hakuna budi adhabu zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka agizo hilo.

Alifahamisha kuwa baadae ZRA itawaangalia kwa kina wananchi ambao wanashindwa kudai risiti za kielektroniki huku akiwasihi kujenga utamaduni wa kudai risiti kwani watakuwa wameichangia serikali katika ulipaji wa kodi. 

Hata hivyo, alisema katika ziara hiyo wamebaini wapo ambao wafanyabiashara wanatumia mashine za elektroniki vizuri jambo ambalo linaendelea kuimarisha ulipaji wa kodi.

“Tunawapongeza wale wafanyabiashara ambao wanatoa risiti za kielektoniki kwa wateja na kuwaomba kuendeleza utamaduni huo umbao unaleta maslahi mapana ya nchi”, alisema.

Alifahamisha kuwa ziara hiyo itakuwa endelevu na itafanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mlandege na Mchangani Mjini.

Nae mfanyabiashara Issa Salum Omar alisema kuwa changamoto kubwa inayopelekea baadhi ya wafanyabiashara kutozitumia mashine za kielektroniki ni pamoja na kuwepo kwa mazingira magumu ya kibiashara.

Aliishauri ZRA kwamba ni vyema kutafuta eneo lenye mzunguko mzuri wa kibiashara huku akidai kwamba waendelee kupewa muda wa ziada.

Kwa upande wa Mfanyabiashara Habibu Omar Juma alisema kuwa kitendo cha serikali kuweka mashine hizo ni jambo la msingi huku akishauri wafanyabiashara wengine kuheshimu sheria na kanuni zilizopo.

“Mimi sioni sababu kwa baadhi ya wafanyabiashara kuleta mivutano wala kutozitumia mashine hizi kwani hazikwamishi wala kukwaza utendaji wetu”, alisema.

Aidha mfanyabiashara Fatma Saleh Nassour alipongeza serikali kwa kuleta mashine hizo kwani zitasaidia kuwatambua wanaokwepa kufuata sheria sambamba na kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake.

“Nafurahi sana ikiwa zinafanyika ziara kama hizi kwani wapo baadhi ya wafanyabiashara bado hawazitumii mashine hizi kwa visingizio sio rasmini na kama sheria ifuate mkondo wake”, alisema.