NA KHAMISUU ABDALLAH, DAR ES SALAM
OFISI ya Msajili wa Hazina Zanzibar, imetiliana saini hati ya mashirikiano na Taasisi ya Uadilifu na Uwajibikaji wa Kifedha Center for Integrity and Financial Accountability (CIFA) Tanzania, kwa lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na ufanisi katika mashirika ya umma.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo ilifanyika katika Ofisi za CIFA, Millennium Towers, Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, alisema kuwa mashirikiano hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa mali za umma unazingatia misingi ya utawala bora.
Alisema lengo kuu la makubaliano hayo ni kuimarisha mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa mashirika ya umma, hususan kupitia kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi na menejimenti ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.
“Tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kufunga mkataba huu na CIFA, hususan katika eneo la mashirika ya umma ili kuzipa nguvu bodi zetu, kufahamu vyema majukumu na malengo yao na hatimae kuongeza ufanisi wa taasisi hizo,” alisema Sanya.
Aidha alibainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati ikiwemo kuingia mikataba ya utendaji kazi na wenyeviti wa bodi za taasisi za umma, hatua inayolenga kupima uwajibikaji na matokeo ya utekelezaji wa majukumu yao.
Alisisitiza kuwa bila kuwepo kwa utawala bora, uadilifu, uwazi na usawa, ni vigumu kufikia ufanisi unaotarajiwa na serikakali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
