Skip to content

Mitaa ya Viwanda Kujengwa Mikoa 11, Vijana Kunufaika

  • Bara

Na Saida Issa,Dodoma

SERIKALI imeweka mkazo mpya katika kusogeza viwanda karibu na wananchi kwa kujenga mitaa ya viwanda na kongani, ambapo tathmini ya awali tayari imekamilika katika mikoa 11, ikiwemo Shinyanga, Tabora na Singida.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga wakati akizungumza na waandishi wa habari na Watanzania kuhusu mafanikio ya siku 100 katika sekta hiyo baada ya uchaguzi mkuu.

Aidha alisema Wizara imeandaa Programu Maalum ya Uwekezaji kwa Vijana kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA)na Shirika la Maendeleo Viwanda Vidogo (SIDO), inayolenga.

“kuwezesha biashara 100,000 zinazoongozwa na vijana kupitia ufadhili jumuishi, miundombinu ya viwanda na uwezeshaji wa biashara nje ya nchi,

“Pia hii inalenga kutekeleza mpango maalum wa kukuza viwanda utakaowezesha ongezeko la viwanda 9,048 na kuzalisha zaidi ya ajira milioni 6.5 katika kipindi cha miaka sita,”alisema.

Aidha alisema hatua hiyo inamaanisha viwanda vinakwenda vijijini na pembezoni hivyo, kipato cha wakulima kinaongezeka kupitia uongezaji thamani, na maelfu ya vijana wanafunguliwa milango ya kumiliki na kuendesha viwanda na biashara ndani ya kongani hizo.

Kadhalika Waziri Kapinga, alisema kuwa ndani ya siku hizo 100 Wizara kupitia BRELA imeweka msukumo mkubwa katika urasimishaji wa biashara na ulinzi wa ubunifu ambapo kampuni 4,233 zimesajiliwa kati ya hizo 2,915 ni za vijana.

Waziri huyo alieleza kuwa mafanikio ya siku 100 ni ishara kwamba wameielekeza Tanzania kwenye njia sahihi ya uchumi wa viwanda, uchumi wa ubunifu na uchumi wa kijani unaomgusa kila Mtanzania, hususan kijana.

“Serikali itaendelea kuimarisha mikopo ya riba nafuu, kurahisisha urasimishaji wa biashara, kujenga na kuendeleza mitaa ya viwanda, kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kutafuta masoko ya kimataifa kwa bidhaa zetu,”alisema.