Na Saida Issa, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga, amepokea msaada wa vifaa vya dharura kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Maafa, kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na mafuriko makubwa yaliyoikumba wilaya hiyo.
Akizungumza jijini Dodoma, Asenga ametoa pole kwa wananchi wote walioathirika na janga hilo, hasa wa maeneo ya Michenga, Lumemo na Lipangalala ambayo yameathirika zaidi.
Amesema kiwango cha maji kilichoshuhudiwa mwaka huu ni kikubwa kuliko ilivyozoeleka katika miaka iliyopita, hali iliyosababisha ongezeko la athari kwa wananchi.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, takribani kaya 100 zimeathirika moja kwa moja, huku idadi ya watu walioguswa na mafuriko hayo ikifikia kati ya 15,000 hadi 16,000. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hadi sasa hakuna kifo kilichoripotiwa.
Msaada uliopokelewa unajumuisha magodoro 75, mablanketi 100 na vyandarua 100. Aidha, mahindi tani 10 yanatarajiwa kuwasili hivi karibuni ili kusaidia upatikanaji wa chakula kwa waathirika.
Asenga amesema msaada huo utasaidia kupunguza makali ya maisha kwa wananchi waliopoteza makazi na mali zao kutokana na mafuriko hayo.
Ametoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu,kwa hatua za haraka walizochukua kuhakikisha misaada inawafikia wahanga kwa wakati.
Pia amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa juhudi kubwa walizozifanya katika kuwaokoa wananchi waliokuwa hatarini, akisema mchango wao umeokoa maisha ya watu wengi.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo amesema ofisi yake inaendelea kutafuta unga ili kusaidia mahitaji ya chakula kwa wananchi walioathirika, huku wakisubiri misaada mingine zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa wabunge wanaendelea kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha na kufukua mabwawa, ili kupunguza au kumaliza kabisa changamoto ya mafuriko nchini.
Kwa sasa, msaada huo uko njiani kuelekea Kilombero, huku Asenga naye akitarajiwa kuwasili eneo hilo kwa ajili ya kushiriki moja kwa moja katika kutoa pole na msaada kwa wananchi wake huku akisema kuwa ofisi yake itachangia unga kwaajili ya kuendelea kuwafatiji waathirika hao.
