Na Saida Issa, Dodoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya maji, hali iliyopelekea kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi katika maeneo mengi ya nchi.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili, akieleza kuwa utekelezaji wa miradi ya maji umeimarika kwa kasi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Aweso alisema kuwa kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha, kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati inayolenga kuhudumia wananchi wa mijini na vijijini kwa wakati mmoja.
Alibainisha kuwa Wizara ya Maji inaendelea kusimamia utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, mradi mkubwa unaolenga kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi kupitia vyanzo vikuu vya maji, ikiwemo Ziwa Victoria, ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa uhakika na endelevu.
Akifafanua zaidi, Aweso alisema mradi huo unafanana na reli ya kisasa ya mwendokasi (SGR), akieleza kuwa wizara yake nayo ina mtandao wa kisasa wa kusafirisha maji kwa umbali mrefu, alioufananisha na “SGR ya maji.”

Alisema maji yanayotoka Ziwa Victoria tayari yameanza kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Tabora, hususan wilaya za Sikonge, Kaliua na Urambo, huku wananchi wa Wilaya ya Sikonge wakiwa miongoni mwa wanufaika wa awali wa mradi huo.
Aweso aliongeza kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya kupeleka maji hayo mkoani Dodoma kupitia mkoa wa Singida, ambapo alieleza kuwa upembuzi yakinifu wa mradi huo tayari umekamilika na hatua inayofuata ni kumpata mkandarasi.
“Tuko katika hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi ili kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuunganisha miradi ya maji katika Gridi ya Taifa, jambo litakaloboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji nchini,” alisema Aweso.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya miradi hiyo yanahitaji uwajibikaji wa dhati kutoka kwa wasimamizi na watendaji wa Wizara ya Maji, akielekeza viongozi kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi badala ya kuwa viongozi wa majina tu.
“Hatutaki viongozi wanaoonekana ofisini bila matokeo. Tunahitaji viongozi wanaosimamia kazi, wanawajibika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufunga mita za malipo ya kabla (prepaid meters) kwenye huduma ya maji, hatua itakayoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutekeleza mfumo huo, akibainisha kuwa ni mageuzi makubwa katika usimamizi wa sekta ya maji.
