Skip to content

Mbarawa Aagiza LATRA, Polisi Wakaze Kamba Kuwalinda Wanafunzi

  • Bara


Na Saida Issa, Dodoma.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuchukua hatua za haraka kusajili na kuthibitisha madereva na makondakta wa daladala, kudhibiti ipasavyo nauli za wanafunzi, pamoja na kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya mabasi ya mijini ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanafunzi.

Maelekezo hayo yametolewa jijini Dodoma wakati Waziri huyo akizungumza na waandishi wa habari, kufuatia kusambaa kwa video mitandaoni inayoonesha mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Mariana Eric Mirindima wa Shule ya Sekondari Jangwani, akiwasilisha barua akieleza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanapotumia usafiri wa daladala.

Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia tabia ya baadhi ya madereva na makondakta kuwanyima au kuwanyanyasa wanafunzi kwa madai ya kutolipa nauli kamili, akibainisha kuwa usalama na haki ya mwanafunzi kupata elimu ni kipaumbele cha Serikali kuliko maslahi ya kibiashara.

Katika maelezo yaliyomo kwenye barua hiyo, mwanafunzi huyo alieleza kuwa baadhi ya makondakta wamekuwa wakikataa kuwabeba wanafunzi, hali inayowalazimu kusubiri vituoni kwa muda mrefu, kuchelewa shuleni au hata kushindwa kabisa kuhudhuria masomo, jambo linaloweka hatarini usalama wao na kudhoofisha maendeleo yao kielimu.

Waziri Mbarawa amempongeza mwanafunzi huyo pamoja na mzazi wake kwa ujasiri wa kuwasilisha malalamiko, akisema Serikali imepokea ujumbe huo na iko tayari kuchukua hatua zinazostahili.

“Hatua hii inaonesha ushiriki wa wananchi katika kusimamia haki zao. Serikali imesikia kilio cha wanafunzi na itakifanyia kazi,” amesema.

Amefafanua kuwa licha ya Serikali kuipa nafasi sekta binafsi kutoa huduma za usafiri wa umma, haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watoa huduma watakaokiuka Sheria, Kanuni na maadili ya utoaji wa huduma, hususan kwa wanafunzi.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Prof. Mbarawa amesema Serikali imeandaa mikakati ya kuboresha usafiri wa wanafunzi mijini, ikiwemo kuanzisha mabasi maalumu kwa ajili ya wanafunzi nyakati za asubuhi na jioni, pamoja na kutenga mabehewa maalumu kwenye treni za mijini, hususan jijini Dar es Salaam.

Aidha, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa nauli maalumu ya Shilingi 200 kwa wanafunzi katika daladala na mabasi yaendayo haraka, sambamba na kutoa elimu kwa watoa huduma na abiria ili kujenga nidhamu, heshima na uwajibikaji katika sekta ya usafiri wa umma.

Serikali pia imewataka wananchi kushiriki kikamilifu kuwalinda wanafunzi kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki zao kupitia namba za bure za LATRA au mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, ili hatua zichukuliwe kwa wahusika.

Waziri Mbarawa ametoa onyo kwa wamiliki wa daladala kuhakikisha watumishi wao wanazingatia Sheria na Kanuni za nchi, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia yeyote atakayebainika kuwanyanyasa au kuwanyima haki wanafunzi.

Kwa mujibu wa Serikali, hatua hizo zote zinalenga kujenga mfumo wa usafiri wa umma ulio salama, wenye heshima na unaolinda haki za wanafunzi, ili kuwawezesha kuhudhuria masomo yao bila hofu wala vikwazo.