ABUJA, NIGERIA
MAREKANI imetuma kikosi kidogo cha wanajeshi nchini Nigeria, ofisa mkuu wa jeshi la Marekani amethibitisha, ikiwa ni mara ya kwanza kukiri hadharani kuwepo kwa vikosi vya Marekani nchini humo tangu ilipofanya mashambulizi ya anga mwishoni mwa mwaka jana.
Mkuu wa kamandi ya Marekani Afrika (Africom), Jenerali Dagvin RM Anderson, alisema alikutana na Rais wa Nigeria Bola Tinubu mjini Roma nchini Italia, ambapo walijadili usalama wa kikanda na hitaji la ushirikiano wa karibu.
Jenerali Anderson alisema nchi zote mbili zimekubaliana juu ya njia ya kusonga mbele katika kulinda amani kwenye ukanda huo unaokabiliwa na hali ya kulegalega kwa usalama.
“Hiyo imesababisha kuongezeka kwa ushirikiano kati ya mataifa yetu, kujumuisha timu ndogo ambayo inaleta uwezo wa kipekee kutoka Marekani ili kuongeza kile ambacho Nigeria imekuwa ikifanya kwa miaka kadhaa”, Jenerali Anderson alisema.
Aliongeza kuwa kutumwa kwa wanajeshi nchini humo kulifanywa kwa ombi la Nigeria na kulenga msaada wa kijasusi.
Hilo linatokea huku kukiwa na shinikizo kutoka Ikulu ya Marekani kwa serikali ya Nigeria kuboresha usalama na kufanya zaidi kulinda jumuiya za kikristo.
Rais Donald Trump hapo awali alidai kuwa kulikuwa na mauaji ya kimbari ya wakiristo nchini Nigeria, akipendekeza kuwa viongozi walikuwa wakishindwa kuwalinda wakristo dhidi ya mashambulizi ya wanajihadi.
Serikali ya Nigeria imekanusha madai hayo, ikisema kuwa waislamu, wakristo na wale wasio na imani sawa wanalengwa na makundi yenye silaha.
Krismasi iliyopita, Marekani ilifanya mashambulizi ya angani katika jimbo la Sokoto nchini Nigeria, ikisema kuwa ilikuwa ikilenga kambi zinazotumiwa na makundi yenye uhusiano na Islamic State.
Tangu wakati huo, Nigeria na Marekani zimeimarisha ushirikiano wa kiusalama, ikiwa ni pamoja na kushirikishana taarifa za kijasusi.
