NA ABOUD MAHMOUD
WAISLAM wenye kuishi na baadhi ya maradhi hawatoruhusiwa kuingia nchini Saudi Arabia kwenda kutekeleza ibada ya hijja kwa mwaka 2026.
Daktari dhamana wa afya za mahujaji, Naufal Kassim Mohammed, ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika msikiti Jamii Zinjibar uliopo Kiembe Samaki.
Aliyataja maradhi hayo ni pamoja na figo linalohitaji kufanyiwa usafishaji, moyo, mapafu yanayohitaji matumizi ya oksijini, maradhi ya ini na uti wa mgongo unaomzuia mgonjwa kufanya shughuli za kawaida.
Maradhi mengine ni mishipa ya fahamu inayosababisha ulemavu wa viungo, uzee, shida ya akili, ujauzito, maradhi ya miguu yanayosababisha mtu kushindwa kutembea kwa masafa na waliopo kwenye matibabu ya saratani.
Alisema kuwa maelekezo hayo wameyapokea kutoka kwa mamlaka inayosimamia ibada ya Hijja kutoka nchini Saudi Arabia, hatua ambayo inalenga kulinda afya za wenye nia ya kwenda kutekeleza ibada hiyo.
Dk. Naufal alikumbushia kuwa miongozo inayotakiwa kufuatwa kwa kila taasisi zinazosimamia mahujaji ni kuhakikisha wanapima afya za mahujaji watarajiwa wakati wa kujiandikisha.
Miongozo mengine kwa taasisi inayochukua mahujaji wa jinsia ya kike na kiume inatakiwa kuwa na madaktari angalau wawili, mmoja kutoka kila jinsia.
Dk. Naufal alitaja muongozi mwengine kujua kwa undani upasuaji wowote aliofanyiwa hujaji na kuangalia kama upasuaji huo utaleta matatizo wakati wa safari.
Pia alisema chanjo kwa mahujaji zisisubiri kukaribia kwa safari na badala yake waanze baada ya kufanya malipo kutokana na kuwa nyengine zinahitaji kukamilika katika kipindi cha miezi sita ikiwemo ya homa ya ini.
Sambamba na hayo daktari huyo dhamana alifahamisha kuwa chanjo ambazo zinategemewa kufanywa na mahujaji ni maradhi yanayotokana na homa ya uti wa mgongo, polio, homa ya ini na homa ya manjano.
Dk. Naufal alisema kuwa ofisi ya Hijja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawasihi viongozi wa taasisi kukubali maelekezo ya madaktari kuhusu afya za mahujaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wakf, Amana na Hijja kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, Madina Haji Khamis alisema kwa Saudi Arabia imekua ikitoa maelekezo yanayohusu utekelezaji wa ibada hiyo.
Alisema maelekezo hayo yameainishwa katika mpango wa muda mrefu wa maendeleo na maono yao ya miaka 15.
Hajat Madina alisema moja ya mambo ambayo serikali ya nchi hiyo imeyapa kipaombele ni kuboresha uratibu na utekelezaji wa ibada hiyo ili kuondoa changamoto zinazowakabili mahujaji kuanzia maandalizi ya hijja kupitia afya za mahujaji.
Naye Kadhi wa Rufaa Mahakama Kuu Zanzibar, Iddi Said Khamis, alisema ibada hiyo inahitaji maandalizi ya kiwiliwili, kiroho na nafsi.
Alieleza kuwa ili hujaji atimize ibada hiyo anahitajika kuwa na nguvu na kujuitayarisha nan a mazingira tofauti na kujiandaa kuwa na maingiliano na watu tofauti na kuwa katika mikusanyiko.
Hata hivyo, aliwataka mahujaji watarajiwa kutafuta elimu ya kutosha ya ibada hiyo na kufanya mwenyewe bila ya kufuata mkumbo.
