NA MAUA ABDULLA, BMMA
MSTAHIKI Meya wa Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’, Chumu Shuwari Machano, amewataka Madereva na Makondakta wa gari za abiria zinazofanya safari katika njia (ruti) za Kijichi – Fuoni na Kijichi – Mjini kufika na kupakia abiria katika kituo cha daladala cha Mndo ili kuepuka ajali.
Meya Machano alitoa maagizo hayo katika ukumbi wa Ofisi za Manispaa Kianga alipokuwa akizungumza na watendaji wa gari ziliokamatwa na Manispaa kwa kosa la kukaidi agizo la kufika katika kituo hicho, hali ambayo imetajwa kuwa chanzo cha ajali za mara kwa mara kutokana na kushusha na kupakia abiria katika maeneo yasiyo rasmi likiwemo la Kijichi chini ya mlima.
Alisisitiza kuwa kitendo cha kupakia na kushusha abiria nje ya vituo rasmi ni hatari kwa usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara hivyo Manispaa haitosita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanaokiuka taratibu hizo.
Kutokana na makosa hayo, Madereva waliobainika walitakiwa kulipa faini ya shilingi elfu 40,000 kwa kila mmoja, hatua inayolenga kutoa funzo kwao na kwa madereva wengine ili kuzingatia sheria na kanuni za usafiri wa abiria.
“Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ limeendelea kusisitiza kuwa litaimarisha doria na usimamizi wa usafiri wa umma ili kuhakikisha usalama wa abiria unalindwa na sheria zinafuatwa kikamilifu”, alieleza Chumu.
Kwa upande wao, madereva na makonda hao walikiri kutenda kosa hilo na kulipa faini iliyotolewa huku wakiahidi kutorudia kutenda kosa hilo katika maeneo yasiyo rasmi kwa lengo la kuepusha ajali zisizokuwa na ulazima.
Miongoni mwa gari zilizotozwa faini hizo ni pamoja na Coaster yenye namba za usajili Z 794 AAE inayoendeshwa na Salum Seif Salum, Coaster Z 448 AAP inayoendeshwa na Suleiman Khalfan Suleiman, Coaster Z 939 LS inayoendeshwa na Ibrahim Bakari Hassan, pamoja na Coaster Z 55 HX inayoendeshwa na Rashid Moh’d Salum.
