ABUJA, NIGERIA
TAKRIBAN watu 30 wamefariki baada ya lori lililokuwa limebeba abiria na mizigo kuanguka katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Nigeria la Kano, mamlaka za mitaa zilisema.
Taarifa zilisema kuwa watu wengingine wengi walijeruhiwa baada ya dereva kushindwa kulidhibiti gari hilo walipokuwa wakisafiri kwenye barabara kuu.
Lori hilo liliacha njia na kuanguka katika kijiji cha Kwanar Barde, kijiji ambacho kinapatikana katika eneo la serikali ya mtaa wa Gezawa.
Msemaji wa gavana wa Jimbo la Kano, Bature Dawakin-Tofa, aliiambia Xinhua kwa njia ya simu, akihusisha kisa hicho na “uendeshaji wa kizembe.”
Gavana wa Jimbo la Kano Abba Yusuf alielezea tukio hilo kuwa la “bahati mbaya,” na akaagiza mamlaka za afya za eneo hilo kutoa huduma za matibabu bila malipo na kwa wakati kwa walionusurika.
Ajali mbaya za barabarani hutokea mara kwa mara nchini Nigeria, mara nyingi husababishwa na upakiaji kupita kiasi, hali mbaya ya barabarani na kuendesha gari kwa uzembe.
