NA MWAJUMA JUMA
KOCHA wa timu ya Mafunzo, Haji Nuhu, amesema ligi kuu ya Zanzibar inaendelea kubadilika na kuonyesha ushindani mkubwa kila uchao, jambo linalohitaji maandalizi ya kutosha kwa kila timu.
Akizungumza baada ya mchezo wao wa ligi dhidi ya Mlandege na kutoka sare tasa, Haji alisema kila siku ligi inazidi kupata nguvu na kuvutia mashabiki wengi kutokana na ubora unaoonekana uwanjani.
“Ligi inabadilika sana, ukiwa hujajiandaa vizuri utakutana na matokeo ambayo hukukutarajia,” alisema.
Aliongeza kuwa kushindwa kupata bao dhidi ya wapinzani wao hakukutokani na makosa, bali kutokana na ubora wa mchezo wenyewe, ambapo kila timu ilicheza kwa umakini mkubwa.
Kocha huyo alisema wachezaji wake walionesha nidhamu na juhudi kubwa uwanjani, lakini bado wana kazi ya kurekebisha baadhi ya maeneo, hasa katika umaliziaji.
Aidha alisema wataendelea kufanya mazoezi kuhakikisha wanapata matokeo bora kwenye michezo ijayo.
