Skip to content

Kura ya mapema yafanyika kwa utulivu

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imesema zoezi la kura ya mapema lililoyahusisha majimbo 50 ya uchaguzi visiwani Zanzibar, limefanyika kwa utulivu hali ya juu.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara ya kutembelea baadhi ya vituo vilivyohusika kupigwa kwa kura hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George Joseph Kazi alisema zoezi hilo limekwenda vizuri.

Alisema zoezi hilo ambalo limewahusisha wapiga kura maalum ikiwa ni pamoja watendaji wa vikosi vya ulinzi na usalama, watendaji wa Tume ya Uchaguzi, wamejitokeza kwa wingi na hata wale waliyoomba kupiga kura hizo nao wamejitokeza na kupiga kura kwa utulivu mkubwa.

Alisema sheria inaelekeza kwamba upigaji wa kura ya mapema unaitaka Tume iweke orodha na kura ya pamoja Oktoba 29 iweke daftari.

“Kama mtu yupo kwenye orodha basi anakuwa moja kwa moja yumo kwenye daftari na anapofika kituoni basi anatoa kitambulisho chake na anagaaliwa kwenye daftari ambapo mawakala wote wanalo,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema hakuna mawakala waliondolewa kwenye vituo vya kupigia kura na wameshuhudia zoezi hili likifanyika kwa uwazi, ambapo pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi leo kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura.

Kwa upande wake, mgombea Uwakilishi jimbo Pangawe, kutoka Chama cha ACT-Wazalendo Omar Said Shaaban, akiwa katika kituo cha kupigia kura Kijitoupele, alisema ni imani yake uchaguzi utakuwa huru na haki, hatua ambayo itakuza demokrasia nchini.

Aliipongeza ZEC kutatua changamoto ndogo ndogo ambazo ziliwasilishwa na chama hicho baada ya kujitokeza katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Naye mgombea udiwani wadi ya Urusi, jimbo la Jangombe, Ishaka Said Hussein alisema hali ya ulinzi na usalama ipo vizuri na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuendeleza amani waliyokuwa nayo na kusubiri matokeo yatakavyokuja kuyapokea vizuri na atakaeshindwa akubali kushinda na atakaeshinda akubali kuwa yeye ni mshindi na tume imtangaze.

Zoezi la upigaji wa kura ya mapema lilianza saa 1:00 asubuhi hadi saa 10 za jioni, ambapo watendaji wa Tume walitembelea baadhi ya vituo vya kupigia kura Tumekuja, Welezo, Kijitoupele na Haile – salasse

ZEC imeendesha kura hiyo kwa wanahusika kwa mujibu wa kanuni ya 40 (1) ya kanuni ya uchaguzi mkuu 2025.