SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati inatarajia kuzindua Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Mtera kilichojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.7, hatua inayolenga kuongeza nguvu na uhakika wa umeme na kunufaisha wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, alisema uzinduzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa umeme katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa pamoja na mikoa ya Dodoma na Iringa kwa ujumla.
Alisema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia Watanzania wote na kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Mradi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwani utaongeza nguvu ya umeme itakayowezesha kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo viwanda vikubwa na vidogo,” alisema Mhandisi Saidy.
Aliongeza kuwa kituo hicho kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Nishati, Deograus Ndejembi na kitawanufaisha moja kwa moja wananchi wa wilaya za Mpwapwa na Kongwa pamoja na wakazi wa vijiji vya Mtera.
Aidha, alisema kukamilika kwa mradi huo kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la umeme hafifu na kukatika kwa umeme mara kwa mara, sambamba na kuimarisha usambazaji wa umeme kutoka Mtera kwenda mikoa ya Dodoma na Iringa.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Saidy alisema Serikali inatarajia kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na huduma ya umeme.
Alibainisha kuwa kupitia mradi huo, wateja wa awali wapatao 250,000 wataunganishwa na huduma ya umeme katika maeneo yatakayopitiwa na mradi.
Mhandisi Saidy alisema kukamilika kwa mradi huo kutabaki na vitongoji 13,900 ambavyo bado havijaunganishwa na umeme, lakini Serikali ina mpango wa kuvifikia vyote kabla ya mwaka 2030.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote 12,318. Kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza mpango mkakati wa kuhakikisha vitongoji vyote vinaunganishwa na huduma ya umeme,” alisema.
