SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo imeanza kutekeleza mkakati wa kujenga maghala ya kisasa ya kuhifadhi chakula ili kuimarisha uhakika wa chakula na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na maafa.
Akizungumza wakati akiwasilisha mikakati ya kugharamia hatari za mabadiliko ya tabianchi, Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula Pemba, Suleiman Atiki Suleiman, alisema ujenzi wa maghala hayo ni hatua ya kimkakati ya kuhakikisha jamii inakuwa salama hata pindi maafa yanapotokea.
Alisema serikali imeamua kuchukua tahadhari mapema kwa kuanzisha miundombinu ya kuhifadhi chakula ili kuondoa hatari ya upungufu wa chakula wakati wa dharura.
Alifafanua kuwa maghala hayo yatahifadhi zaidi vyakula vya nafaka ambavyo ndivyo vinavyotumiwa kwa wingi na wananchi wa Zanzibar, ikiwemo mpunga, mahindi, uwele na mtama.
Aidha, alisema mazao hayo hulimwa ndani ya Zanzibar, lakini endapo mavuno hayatokidhi mahitaji ya chakula na akiba, hulazimika kuagizwa kutoka nje ya visiwa hivyo ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Akitoa takwimu za maghala hayo, alisema wilaya ya Mkoani kuna ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi tani 708.75 za chakula, wilaya ya ChakeChake eneo la Ole Dodeani kuna ghala lenye uwezo wa kuhifadhi tani 650.
Aidha alisema wilaya ya Wete kuna maghala matatu la Weni lenye uwezo wa kuhifadhi tani 560 na mawili yapo Kizimbani yenye uwezo wa kuhifadhi tani za vyakula 323.78 na 323.79.
Alieleza kuwa baadhi ya maghala hayo tayari yameanza kutumika, likiwemo la Ole Dodeani, ambalo limejengwa kupitia mradi wa Sumukuvu chini ya wizara hiyo.
Alibainisha kuwa endapo hakutatokea maafa yoyote, chakula hicho hakitaruhusiwa kukaa hadi kuharibika, bali serikali kwa kushirikiana na wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda itauza kwa wafanyabiashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Alisema utaratibu huo utasaidia kuzungusha akiba ya chakula na kuepusha upotevu pamoja na kuimarisha soko la ndani la mazao ya wakulima.
Sambamba na hayo, alitoa wito kwa wakulima kuendelea kuimarisha kilimo cha nafaka ili kuongeza uzalishaji na kuwezesha maghala hayo kuwa na akiba ya kutosha wakati wote.
“Tunawaomba wakulima wetu waendelee kulima kwa bidii mazao ya nafaka, kwani juhudi zao ndizo zitakazowezesha mpango huu wa uhifadhi wa chakula kufanikiwa”, alisema.
