Skip to content

Kikosi cha Zimamoto chapokea gari, boti za uokozi

  • Zanzibar

NA TATU MAKAME

KIKOSI cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, kimepokea gari tisa na boti moja kutoka nchini Austria, ambazo zitatumika kuzimia moto katika maeneo mbalimbali vifaa vyote vikiwa vimegharimu shilingi bilioni 16.22.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Kilimani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Kamishna wa Kikosi hicho Rashid Mzee Abdalla alisema gari hizo ni mkopo wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia benki ya Reinforcement ya Austria.

Alifahamisha kuwa gari hizo tisa zilizoingia kwa awamu ya pili, gari tatu za maji zenye ujazo wa lita 15,000, gari mbili za ngazi ambazo zitatumika kufanya uokozi kwenye jumba refu, gari nne zenye ujazo wa lita 5,000 kila moja na kutumika kwenye manispaa na mabaraza ya miji pale yanapotolea majanga ya moto na boti ambayo itatumika katika shuhuli za uokozi baharini.

Alisema gari hizo tisa zinatimiza idadi ya gari 19 zilizofika nchini kupitia mkopo huo ambazo zitapunguza majanga ya moto katika maeneo mbalimbali.

Alifafanua kuwa gari mbili kati ya 21 zinamalizia kutengenezwa nchini humo na muda mfupi zitaingia nchini baada ya matengenezo.

Alisema lengo la kununua gari hizo ni kupunguza majanga ya moto hapa nchini katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, ambayo yamekuwa yakiongezeka.

Alifahamisha kuwa gari hizo pia zitakuwa na uwezo wa kuunganisha pampu moja kwa moja kupitia visima vya kikosi hicho pale maji yanapomaliza wakati zoezi la kuzima moto linapoendelea.

Aidha aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kikosi hicho pale yanapotokea majanga ya moto kwa kupiga sim ya kikosi hicho 114.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi kuacha nafasi wakati wanapojenga nyumba za makaazi ili kurahisisha uzimaji wa moto.

Kwa upande wao wananchi waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi inayochukua katika kutafuta ufumbuzi wa majanga ya moto ikiwemo kutafuta vifaa vya kuzimia moto.

Gari hizo zilizonunuliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mkakati wa kupunguza majanga ya moto katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.