Skip to content

Kampuni kutumia 203.9bn/- uwekezaji viwanda

NA MARYAM NASSOR

KAMPUNI zinatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 203.906 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mitatu ya uwekezaji wa viwanda hapa Zanzibar.

Miradi hiyo ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha dawa za magonjwa ya binadamu, kiwanda cha nguo pamoja na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma.

Hayo yameelezwa na kaimu waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Shariff Ali Shariff, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa siku 100 tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aingie madarakani kwa awamu ya pili.

Waziri huyo alisema kuwa, viwanda hivyo vitajengwa katika eneo la Dunga Zuze ambapo tayari miradi ya ujenzi wa viwanda imeshaanza kutekelezwa.

Akifafanua zaidi alisema kuwa kiwanda cha kuzalisha dawa za magonjwa ya binadamu kinachomilikiwa na kampuni ya Afrika Bichem Pharma Co. Ltd, kiwanda cha nguo cha Mama Afrika Textile Ltd pamoja na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma vilivyo chini ya mmiliki Fabricated Metal Works.

“Pamoja na mambo mengine lakini wizara hii ina jukumu la kukuza maendeleo ya viwanda pamoja na kusimamia na kuimarisha mazingira mazuri ya ufanyaji biashara, sambamba na kuhakikisha uwepo wa masoko ya bidhaa za ndani katika masoko ya nje ya nchi”, alisema.

Alieleza kuwa, miongoni mwa viashiria vinavyotumika kupima maendeleo ya nchi duniani ni ukuaji wa sekta ya viwanda, na kwamba kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM, Serikali imefanikiwa kuimarisha sekta hiyo kwa kuvutia uwekezaji katika maeneo tengefu ya viwanda.

Waziri Shariff aliyataja maeneo hayo tengefu ya uwekezaji kuwa ni pamoja na Dunga, Chamanangwe na Pangatupu.

Aidha alisema kuwa, kuimarika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa kutoka asilimia 20.8 ya sasa hadi kufikia asilimia 25 ifikapo mwaka 2030. Pia miradi hiyo itachangia kupatikana kwa ajira, kupunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuimarisha biashara nchini.

Alisema, wizara kupitia Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata mwani katika eneo la Chamanangwe, Mkoa wa Kusini Pemba. Mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza thamani ya zao la mwani.

Sambamba na eneo la viwanda, lakini Waziri Shariff alisema wizara kupitia taasisi yake ya Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar (ZFCC) inaendelea kudhibiti bei elekezi kwa bidhaa muhimu zikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari, mafuta ya kula na saruji.

Alieleza kuwa, katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais wa Zanzibar, jumla ya maduka 375, maghala 18 na ‘supermarket’ nne zimekaguliwa, ambapo wafanyabiashara tisa walibainika kukiuka sheria kwa kutoweka bei za utambulisho katika bidhaa zao.

Shariff aliongeza kuwa, wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango iko katika hatua za maandalizi ya kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kumbi za Mikutano na Maonesho ya Biashara katika eneo la Fumba chenye ukubwa wa hekari 10.7.

Alisema kituo hicho kinatarajiwa kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuunganisha biashara na sekta muhimu zikiwemo utalii, fedha, mawasiliano, miundombinu, elimu, afya na kilimo pamoja na kukuza biashara za ndani.