Na Saida Issa, Dodoma
Kuelekea msimu wa nne wa mashindano ya Bunge Bonanza yanayotarajiwa kuchezwa Januari 31, 2026 katika viwanja vya John Merin jijini Dodoma, hali ya ushindani na hamasa imeanza kushika kasi, huku mashabiki wa Simba SC na Young Africans SC wakianza kuoneshana ubabe mapema.
Mashabiki wa vigogo hao wa soka nchini walikutana katika viwanja vya Bunge, ambapo walitumia fursa hiyo kubadilishana kauli za ushindani, kueleza maandalizi yao pamoja na matarajio makubwa kuelekea bonanza hilo linalowakutanisha wabunge na wananchi katika burudani ya michezo.
Katika mkutano huo, kila upande ulionekana kujiamini, huku mashabiki wa Simba wakikumbusha ubingwa walioutwaa katika msimu uliopita, wakati wenzao wa Yanga wakiahidi kulipa kisasi na kurejesha heshima yao katika toleo la mwaka huu.
Kamati ya Bunge Bonanza ilianzisha utaratibu wa kuwakutanisha mashabiki wa timu hizo kongwe pamoja na wawakilishi wao Bungeni kama sehemu ya kuimarisha mshikamano, kukuza burudani ya michezo na kuendeleza mahusiano mema kati ya viongozi na wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, alisema maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri, huku mwitikio wa mashabiki ukiwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Sanga alibainisha kuwa mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ari iliyooneshwa na mashabiki pamoja na timu shiriki, akisisitiza kuwa lengo la bonanza hilo ni kuhamasisha umoja, afya na mshikamano kupitia michezo.
Aidha, alisema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo, jambo linalozidi kuongeza hadhi na mvuto wa Bunge Bonanza kwa mwaka huu.
Kwa dalili za awali, Bunge Bonanza 2026 linatarajiwa kuwa la aina yake, huku macho na masikio ya wadau wa michezo yakielekezwa Dodoma kushuhudia burudani, ushindani na mshikamano unaojengwa kupitia michezo.
