Skip to content

Hakuna meli iliyopewa leseni kufanya biashara haramu – Dk. Khalid

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hakuna meli yoyote ya kigeni iliyopewa kibali cha kufanya vitendo vya ukiukwaji wa sheria ikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed alieleza hayo wakati akijibu masuala ya wanahabari katika mkutano wa siku 100 wa uongozi wa Rais Dk. Mwinyi uliofanyika ukumbi wa Sanaa Rahaleo.

Dk. Khalid alisema kuwa hivi karibuni kulisambaa taarifa zilizorushwa mitandaoni ya kukamatwa kwa meli ya kigeni huko El Salvador ambayo iliyodaiwa kusajiliwa Zanzibar, jambo ambalo Dk. Khalid alisema bado wanafuatailia ili kujua taarifa sahihi za tukio hilo katika vyombo vyenye mamlaka ikiwa ni pamoja na wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Ni kweli meli hiyo imesajaliwa Zanzibar na serikali inatoa leseni kwa ajili ya kufanya biashara halali baada ya mmiliki wa meli kukidhi vigezo vilivyopo kisheria”, alisema.

Aidha Dk. Khalid alisema mara baada ya serikali kupitia mtandao wa kijamii Febuari 17 kugundua meli iliyosajiliwa Zanzibar kuhusika na tuhuma ya kusafirisha dawa za kulevya ilisikitishwa na hatimae kuchukua hatua za haraka ili kukomesha kitendo hicho.

“Tulipoona katika mtandao wa kijamii tu hapo hapo tulianza kuchukua hatua za kufatilia kwa karibu suala hilo kama inavyotakiwa na IMO na kumtaka ‘Interpol’ kufatilia na jibu amesikia na amefatilia lakini hajapata uthibitisho juu ya suala hilo pia tulimuagiza RO wetu aliopo Balamu alieleza analifahamu kwa kulisikia mitandaoni tu”, alieleza.

Aidha, Dk. Khalid alisema meli zilizosajiliwa Zanzibar zinapokamatwa kwa kuhusika na vitendo vya usafirishaji wa madawa ya kulevya serikali inakasirika sana hasa ikizingatiwa zinasababisha kuichafua bendera ya nchi.

“Hatupendi wala kusika kama kuwa baadhi ya wafanya biashara wanaotumia bendera yetu ya Zanzibar wanafanya vitendo vya ovyo kwani wanatuchafulia bendera yetu,” alisema.

Hata hivyo, Dk. Khalid aliweka wazi miongoni mwa hatua za haraka zilizochukuliwa na serikali kufuatia kadhia hiyo alisema ni pamoja na kufuta usajili na kumtaka alipe faini ya dola 20,000.

Akizungumzia kuhusiana na usajili wa meli za kigeni kwa ujumla, Dk. Khalid alisema serikali imelazimika kuzifutia leseni meli 396 kwa kukiuka utaratibu wa masharti na sheria za usajili ikiwa ni pamoja na kufanya vitendo vya uharamia, usafirishaji bidhaa haramu nakadhalika.

Mbali na hilo, alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana na Kampuni ya Mariten Expact ili kuhakikisha inaziondoa meli zote zinazoweza kuleta athari.

Katika hatua nyengine Dk. Khalid alisema suala kama hilo pia hutokezea katika nchi zote duniani zinazotoa usajili wa meli za kigeni kutokana na wamili kutokuwa waaminifu.