Skip to content

Gari jipya la zimamoto kufika februari 9

  • Bara

Serikali imethibitisha kuwa Jimbo la Katoro linatarajiwa kupokea gari jipya la zimamoto na uokoaji ifikapo tarehe 09 Februari, 2026, hatua inayolenga kuimarisha huduma za dharura na usalama wa wananchi, kufuatia swali la Mbunge wa Katoro, Eng. Kija Limbu Ntemi, lililoulizwa bungeni kuhusu upatikanaji wa gari hilo.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Patrobas Katambi, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kwa kulipatia vitendea kazi vya kisasa ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Waziri Katambi ameeleza kuwa katika jitihada hizo, Jimbo la Katoro tayari limepatiwa gari moja jipya la kuzima moto na uokoaji aina ya IVECO, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto na dharura nyingine katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa kwa sasa gari hilo lipo Mkoani Dar es Salaam na maandalizi ya mwisho yanaendelea kabla ya kusafirishwa kwenda Kanda ya Ziwa. Kwa mujibu wa Waziri, gari hilo linatarajiwa kuwasili Mkoani Geita tarehe 09 Februari, 2026, tayari kwa kuanza kutoa huduma.

Hatua hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Jimbo la Katoro, huku Serikali ikisisitiza kuwa itaendelea kuboresha miundombinu na vifaa vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha huduma za zimamoto na uokoaji zinapatikana kwa wakati na kwa ufanisi katika maeneo yote ya nchi.