Skip to content

Dk. Samia: Ujenzi matenki ya mafuta utaimarisha miundombinu ya usafirishaji

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta katika bandari ya Dar es Salaam na kueleza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji.

Dkt. Samia alisema katika nafasi ya ushindani kama kitovu cha biashara ya kikanda. mradi huo pia utasaidia kudhibiti changamoto za muda mrefu za kupokea na kuhifadhi mafuta, huku ukilenga kuongeza usalama wa nishati nchini.

Akitaja maboresho yanayoendelea bandarini, Dk. Samia alisema ushirikishwaji wa sekta binafsi umeongeza ufanisi, kupanua uwezo wa kuhudumia shehena na kuongeza mapato ya serikali na kuongeza kuwa matanki hayo yatapunguza ucheleweshaji wa shehena, kuongeza upatikanaji wa mafuta kwa wananchi na kuimarisha sekta za uzalishaji.

Aidha aliagiza kuimarishwa kwa Akiba ya Kimkakati ya Hifadhi ya Mafuta na mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa shehena kutoka bandarini hadi hatua za usambazaji, kwa lengo la uwazi na kulinda mapato ya Taifa.

Awali Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, alisema serikali inaendelea kuunganisha huduma za bandari na Reli ya Kisasa (SGR), huku usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ukiwa utakapofunguliwa rasmi.

Aidha, alieleza kuwa bandari kavu zitaanzishwa katika mikoa ya Morogoro, Dodoma na Shinyanga ili kurahisisha mtiririko wa mizigo na kupunguza msongamano bandarini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, alisema kukamilika kwa mradi kutapunguza muda wa kuhudumia meli za mafuta kutoka wastani wa siku 22 hadi 7 kwa meli moja.

Alifafanua kuwa hatua hiyo itapunguza gharama ya Dola za Marekani 25,000 (sawa na shilingi Milioni 58) inayolipwa kwa ucheleweshaji, kuongeza idadi ya meli na hivyo kuimarisha mapato ya Taifa.

Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Bandari, uliolenga kuongeza ushindani, ufanisi na mchango wa sekta ya bandari katika uchumi wa Taifa, pamoja na kuimarisha hadhi ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango la nishati kwa nchi jirani.