Skip to content

Dk. Mwinyi: Tutaweza kwenye uchumi wa kidijitali

RAIS wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaweka kipaumbele kikubwa katika uendeshaji wa uchumi, utoaji wa huduma katika taasisi za umma pamoja na ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

Dk. Mwinyi ameyaeleza hayo alipokutana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Angellah Kairuki ambaye aliambatana na na watendaji wakuu wa wizara hiyo waliofika Ikulu.

Alisisitiza wizara hiyo kufanyakazi kwa ukaribu na Zanzibar kupitia wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu na kuimarisha ushirikiano ili kufanikisha masuala ya muungano yanayosimamiwa na wizara hizo, ikiwemo huduma za posta na tume ya taarifa binafsi.

Alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana Tanzania bara, hususan katika usimamizi wa matumizi ya mifumo ya kidijitali, hivyo ni vyema kutumia fursa hiyo kuijengea uwezo zaidi Zanzibar kwa kuimarisha miundombinu, utaalamu na kuwajengea uwezo watendaji katika sekta mbalimbali.

Dk. Mwinyi alifahamisha kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kuwekeza katika eneo hilo muhimu la undeshaji wa uchumi wa kidijitali ili kuendana na muelekea wa uchumi wa dunia ambao kwa sasa unauendesha na mifumo hiyo.

Aidha ameishauri wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuharakisha ujenzi wa kituo cha ukusanyaji taarifa (data center), hapa Zanzibar kutokana na umuhimu wake katika maendeleo yataifa na mageuzi ya kidijitali.

Alisema ni lazima kuchukua hatua za zaiada ili kufikia kasi kubwa ya upatikanaji wa mawasiliano ya intaneti pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano katika mkongo wa taifa.

Dk. Mwinyi alisisitiza wizara hiyo kuongeza ushirikiano na taasisi za Zanzibar ikiwa ni pamoja na Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) na Mamlaka ya serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ), kwa kuzijengea uwezo, kuimarisha miundombinu.

Naye waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki alimuhakikishia Dk. Mwinyi ushirikiano wa dhati na kufanyakazi kwa ukaribu na wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu na kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika na salama.