Skip to content

Dk. Mwinyi: Tutaongeza fursa kwa vijana

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwapatia elimu bora na kuongeza fursa za mikopo.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo wakati alipozungumza na vijana wa Vyuo Vikuu na makundi mbali mbali ya vijana, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kampasi ya Tunguu.

Akiwa kwenye muendelezo wa kampeni za kuwania urais katika uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka huu, Dk. Mwinyi aliwahakikishia vijana hao kwamba serikali itatanua wigo wa utoaji mikopo hadi kwa wanafunzi wa ngazi ya diploma.

“Nyinyi vijana ndiyo viongozi, na ni kundi muhimu sana kwani zaidi ya asilimia 65 ya wapiga kura wote ni vijana. Hivyo ni lazima mjengewe uwezo ili mpate elimu bora,” alisema.

Alisema serikali ya awamu ya nane ilipoingia madarakani miaka mitano iliyopita ilikuta bajeti ya elimu iko chini ambapo hivi sasa imeongezwa hadi kufukia shilingi bilioni 864.

“Hivyo kipaumbele cha kwanza tulichotoa ni elimu, kwa sababu tunataka vijana wetu katika nchi hii waelimike, kwani taifa linahitaji wataalamu wa baadae,” alisema.

Akizungumzia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, Dk. Mwinyi alisema ilikuwa ni shilingi bilioni 13, ambapo hadi kufikia mwaka huu wa 2025 bajeti hiyo imepanda hadi kufikia shilingi bilioni 37.

Dk. Mwinyi, alisema serikali ilifanya maamuzi ya makusudi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya diploma ambapo tayari vijana 3,500 wa ngazi hiyo wanapatiwa mikopo hiyo.

Aliahidi kuwa serikali itaendelea kuwajengea uwezo kielimu kuanzia ngazi zote sambamba na kuendelea kujenga Vyuo vya Mafunzo Amali, ili vijana wanaokosa kuendelea elimu ya juu waweze kupata elimu ya ufundi.

Alisema, kundi la vijana lina umuhimu wa kipekee katika kufanya maamuzi au hatma ya uongozi nchini kwa sababu idadi kubwa ya wapiga kura Zanzibar ni vijana.

Alisema, serikali ya Chama cha Mapinduzi inatoa upekee maalum kwa masuala yote yanayohusu vijana na wanachotaka ni kupata fursa ambazo zipo katika maeneo matatu ambayo ni elimu, ajira na fursa ya uongozi.

Aidha Dk. Mwinyi aliwahakikishia vijana hao kuwa katika awamu ya pili akipata ridhaa basi serikali yake itavuka lengo la kutoa ajira zaidi ya ajira 350,000 kwa vijana.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed (Dimwa), aliwataka vijana kuhakikisha wanawahamasisha vijana wenzao kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29.

Alisema, vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhimizana kuhusu swala la amani, umoja na mshikamano kwa mustkabali mpana wa maisha yao ya sasa na ya baadae.