NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru serikali ya Oman kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar kwenye miradi mbalimbali inayosaidia kuchangia maendeleo.
Dk. Mwinyi ameyaeleza hayo kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Said Salim Al-Sinawiy, iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na uhusiano wa kidugu na kwamba mahusiano hayo yataendelea kuimarishwa.
Alifahamisha kuwa misaada inayotolewa na Oman kwa Zanzibar katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, utalii, urithi wa Mji Mkongwe na utamaduni imekuwa nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo, kuihakikishia Oman kuwa Zanzibar itaendelea kudumisha ushirikiano wa karibu kwa maslahi ya wananchi na maendeleo ya pande zote mbili.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwasihi waumini wa dini ya kiislamu pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi na dunia amani.
Alisema machafuko na mifarakani miongoni mwa mataifa husababisha athari mbalimbali, hivyo waumini wanapaswa kuhakikisha wanaiombea amani kwa ajili ya ustawi wa ulimwengu.
Vilevile alimshukuru Balozi wa Oman kwa kuendeleza utaratibu wa kuandaa futari hiyo kila ifikapo mwezi mtukufu wa Ramadhani, hatua ambayo imekuwa ikiwaunganisha watu na kuimarisha umoja na upendo.
Kwa upande wake, Balozi Said Salim Al-Sinawiy alimuhakikishia Dk. Mwinyi kuwa Oman itaendelea kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya Zanzibar, sambamba na kudumisha uhusiano na mashirikiano.
Balozi huyo alimpongeza Dk. Mwinyi kwa uongozi wake unaoleta maendeleo makubwa na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar katika sekta za utalii, elimu, uchumi wa buluu, urithi wa Mji Mkongwe na utamaduni.
