NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali zitakazohakikisha muhimili wa mahakama unatekeleza majukumu yake katika mazingira yanayoakisi utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Makamu wa Pili ameyaeleza hayo alipomuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria Zanzibar yaliyofanyika Wete.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 13.6 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama yaliyoekwa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na mifumo ya TEHAMA.
Alieleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika matumizi ya TEHAMA kuelekea serikali mtandao, ili kutimiza azma ya kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu hasa katika matumizi ya mfumo wa usimamizi wa mashauri na mifumo mengine itakayozidisha uwajibikaji katika upatikanaji wa haki.
Alieleza kuwa kupitia mfumo huo usajili wa mashauri utakuwa rafiki, usikilizaji na uamuzi wa mashauri utafanyika kwa haraka, upatikanaji sahihi wa takwimu, kuongezeka kwa uwazi na kukuza uwajibikaji miongoni mwa wadau wa sheria.
Makamu wa Pili aliupongeza uongozi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kuifanyia kazi sheria ya mwenendo wa wa Madai ya Zanzibar (Civil Procedure Decree Chapter 8) ya mwaka 1917, ambapo rasimu ya sheria mpya na kanuni kadhaa zimeshatayarishwa.
Aliwakumbusha watendaji wa Mahkama kwamba umuhimu wa sheria hiyo kwani ndiyo inayobeba mustakbali wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kuwa ustawi wa kibiashara na uwekezaji mambo ambayo yanategemea ubora wa sheria hiyo.
Akitoa salamu za Mahkama Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla alisema matumizi ya TEHAMA yataleta mageuzi makubwa ya kiutendaji kwa kufanya kazi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika kufikia upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Jaji Khamis alisema mifumo mitano imeundwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wa mahkama ikiwemo mfumo wa usimamizi wa mashauri ambao utazifanya mahkama kuondokana na matumizi ya makaratasi na mawakili watafungua mashauri ya kesi bila ya kufika mahakamani.
Aidha, alifahamisha kuwa mafunzo ya utumiaji wa mifumo hiyo yanaendelea kutolewa kwa watumishi na wadau wa sheria hapa Zanzibar, mafunzo ambayo yataleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za kimahkama Zanzibar.
Jaji Mkuu aliitaja mifumo inayotumiwa na Mahkama za Zanzibar kuwa ni pamoja na mfumo wa usimamizi wa mashauri, mfumo wa ZAN-WAKILI, Mfumo wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, Mfumo wa Malalamiko na utoaji wa maoni na mfumo wa uhifadhi wa hukumu za Mahakama.
Kwa upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Haroun Ali Suleiman, alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na watendaji wa Mahkama katika kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora, wezeshi na salama.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Mwinyi Talib Haji alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuipa kipaombele mahkama katika kuboresha na kujenga miundombinu ya kisasa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Mgeni Jailani Jecha alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuboreshwa mifumo ya Mahkama ili kuendana na kasi ya utendaji wa kazi kwa haki na uwazi.
Kwa upande wake, rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar, Joseph Magazi, amesema utoaji wa haki unahitaji kuendana na matumizi ya TEHAMA katika upatikanaji wa haki, kurahisisha ufikiwaji wa elimu ya sheria na kupanua wigo wa ufahamu wa sheria kwa wananchi.
