RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mabadiliko ya sera na sheria na miongozo ya uwekezaji nchini yametoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuanzisha miradi inayogusa maisha ya watu.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Dk. Mwinyi amesema hayo alipozindua boti mpya ya usafirishaji abiria ya Kilimanjaro IV (dragon of the sea), inayomilikiwa na kampuni ya Azam Marine Ltd, hafla iliyofanyika Mtoni.

Alisema mabadiliko ya kisera na kisheria kwenye uwekezaji yaliyofanywa lengo lake ni kuhakikisha yanachochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi, kuongeza ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa abiria na mizigo.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa serikali inalenga kutoa nafasi kwa wawekezaji wa ndani na nje kukuza utoaji huduma bora kwa wananchi, huku juhudi zikiendelea kuchukuliwa katika kuimarisha miundombinu ya bandari mbali mbali nchini.
“Hatua ya kampuni ya Azam Marine kuwekeza katika sekta ya usafiri itasaidia kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji ya shughuli za usafiri na usafirishaji hapa nchini”, alisema Dk. Mwinyi.

Alibainisha kuwa sekta ya usafiri ina umuhimu katika kukuza maendeleo ya nchi, hivyo serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Sambamba na hilo, Dk. Mwinyi alisema serikali itaendelea kukuza huduma na kuhakikishia inafanya mapitio ya kodi mbali mbali ili kutoa unafuu kwa lengo la kuwafanya wawekezaji watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi alifahamisha kwamba sekta ya usafiri wa baharini ni muhimu sana katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kwani zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayotoka na kuingia nchini inapitia kwa njia ya bahari.
Kuhusu ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani alisema tayari umeshaanza na mategemeo ni kujumuisha sehemu ya meli za mizigo ya makontena, sehemu ya kupokea meli za mafuta na gesi na eneo la chelezo kwa huduma za matengenezo ya meli.
Alisema katika hatua nyengine serikali inaendelea ujenzi wa bandari ya Fumba na bandari nyengine Unguja na Pemba ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka nchini.
Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wawekezaji wazawa kuiga mfano wa Bakhresa kwa kuwa wazalendo na kujali maslahi ya nchi yao.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Marine, Abubakar Aziz Salim alisema boti hiyo imetengenezwa nchini China imegharimu dola milioni 12 na ina uwezo wa kuchukua abiria 631.
Alieleza kuwa kuwasili kwa boti hiyo kutaongeza nguvu ya kusafirisha abiria na kuwaondoshea usumbufu.
Alifahamisha kuwa Kampuni ya ya Azam Marine, ilianza shughuli za usafirishaji mwaka 1992, ambapo hadi sasa kupitia boti zao wana uwezo wa kusafirisha abiria 13,000 kwa siku.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Saleh Saad Mohammed, alisema kuzinduliwa kwa boti hiyo kutasaidia kurahisisha huduma ya usafiri kwa wasafiri wa Unguja, Pemba na Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo aliwaomba wawekezaji wote kuendelea kuzitumia fursa zilizopo nchini kwa ajili ya uwekezaji.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi itaendelea kuhakikisha kuwa kupitia sera yake ya uchumi wa buluu inaweka vivutio vitawahakikisha wawekezaji wanaoleta mitaji yao nchini inaleta faida katika sekta hiyo.

