NA HAFSA GOLO
IMEELEZWA kuwa bandari mpya ya abiria na mizigo ya Mpigaduri inatarajiwa kuzindua mwishoni mwa mwaka huu baada ya kukamilika.
Mkurugenzi Mipango na Uwekezaji, Ali Seif Ali, alieleza hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Malindi Unguja na kusema hatua hiyo inalenga kuimarisha miundombinu ya usafiri baharini, kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi katika visiwa vya Zanzibar.
“Bandari hii mpya ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuimarisha sekta ya usafiri, usafrishaji na biashara ya baharini”, alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema bandari hiyo itaongeza mapato ya serikali ambapo kwa mwezi inakadiriwa kukusanya wastani wa shilingi bilioni moja na kuajiri wastani wa vijana 100 hadi 150 ambao watakuwa ni sehemu katika uendeshaji wa shughuli mbali mbali za bandari hiyo.
“Katika bandari hii mpya ya Mpigaduri watanufaika vijana wengi na ajira za moja kwa moja na zile za muda ikiwa ni pamoja na madereva, wachukuzi, watu wa usafi na wafanyabiashara ndogondogo”, alisema.
Akizungumzia utoaji wa huduma, Ali alisema bandari hiyo itatoa huduma za kisasa ndani ya masaa 24 na haitokuwa na msongomano wa meli kufuatia uwezo wa gati lake na kina kirefu cha maji chenye urefu wa mita tano hadi sita.
Alifahamisha kuwa bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kufunga meli nne za roro kwa wakati mmoja bila ya kuwepo kwa changamoto yoyote na kutaja miongoni mwa meli zitakazofunga gati kwenye bandari hiyo ni pamoja na Azam See Link, Ikram, Azam Comoro na MV Mapinduzi II.
Hata hivyo, alisema serikali bado inaendelea kuboresha huduma za usafiri katika bandari ya Zanzibar ili kuendana na utoaji wa huduma za kiteknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumzia kuhusu usalama, Mkurugenzi huyo alieleza kwamba bandari hiyo itaendeshwa na mifumo ya kisasa ya teknolojia sambamba na kuthibiti uvujaji wa mapato.
“Vitendo vya rushwa na urasimu havitajitokeza katika utoaji wa huduma hasa ikizingatiwa miundombinu ya kisasa itakayotumika katika bandari hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kuzuia uvujaji wa mapato”, alisema.
Nae Mfanyabiashara Nassour Jafar Mazrui, alieleza furaha na matumaini juu ya uzinduzi wa bandari mpya ya Mpigaduri huku akitilia mkazo kuwa mradi huo utarahisisha shughuli zao za biashara na kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa.
Aliongeza kuwa bandari hiyo itakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwani itarahisisha upokeaji wa mizigo kwa wakati na kuongeza ushindani katika sekta ya usafirishaji.
Kwa upande wake Aliy Majid Aliy alisema kuwa bandari hiyo itapunguza changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo na gharama kubwa ya usafiri, lakini kwa kuwepo bandari hiyo mpya, ni wazi ikuwa huduma bora na za kisasa zitachochewa na ufanisi wa kazi.
Aliishukuru serikali kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati kama hiyo, kwani ni ishara ya kujali maendeleo ya wananchi na ustawi wa biashara visiwani.
