NA HAFSA GOLO
NAIBU Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, ameanza ziara yenye lengo la kukagua na kuimarisha utendaji kazi wa vyombo vya usalama pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili watendaji.
Ziara hiyo inalenga kujionea hali halisi ya utoaji huduma kwa wananchi, kiwango cha utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kutathmini mahitaji ya msingi yanayohitajika katika kuboresha sekta ya usalama nchini.
Katika ratiba yake, Naibu Waziri huyo anatarajiwa kutembelea vituo vya polisi, taasisi za magereza na ofisi za Idara ya Uhamiaji, ambako atafanya mazungumzo na maofisa na askari wa kada mbalimbali.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi alipofika kujitambulisha, Ayoub alisema serikali imejipanga kuendelea kuimarisha sekta ya usalama kwa kuhakikisha watumishi wake wanapatiwa vifaa vya kisasa, mafunzo endelevu pamoja na kuboreshewa mazingira ya kazi.
Alisema dhamira ya serikali ni kuendelea kuimarisha taasisi zake za ulinzi na usalama ili ziweze kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadae, sambamba na kulinda misingi ya amani, sheria na utawala bora.
Alisisitiza kuwa uwekezaji katika sekta hiyo ni nguzo muhimu katika kulinda amani, utulivu na ustawi wa taifa.
“Dhamira ya serikali ni kuona vyombo vyetu vya usalama vinafanya kazi katika mazingira bora na kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi na weledi katika kuwahudumia wananchi na ziara hii ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu”, alisema.
Alibainisha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha usalama wa nchi, bado kuna haja ya kuendelea kusikiliza maoni ya watendaji waliopo mstari wa mbele ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho zaidi, ikiwemo miundombinu, rasilimali watu na vitendea kazi.
Aliwataka wananchi kuendeleza ushirikiano na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu viashiria vya uhalifu au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Alisema usalama ni jukumu la pamoja linalohitaji mshikamano kati ya Serikali na jamii.
“Tunasisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama, kwani taarifa zao zina mchango mkubwa katika kuzuia na kupambana na uhalifu, ushirikiano huu ndio msingi wa kudumisha amani na utulivu tulionao,” alibainisha.
Ziara hiyo ya siku mbili inatarajiwa kuhitimishwa kwa mkutano wa majumuisho utakaowakutanisha viongozi wa vyombo vya usalama na wadau mbalimbali, kwa lengo la kujadili matokeo ya ziara hiyo na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Naye Mkuu wa Mkoa huo Moh’d Ali Abdallah alisema ujio wake utaongeza mashirikiano ya kiutendaji hasa katika suala la ulinzi na usalama katika nchi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane inaendelea kuimarisha miundombinu ya ulinzi na usalama na wananchi wanafanya shughuli zao bila ya matatizo yoyote.
