Skip to content

Ajali barabarani zaendelea kukatisha uhai

  • Zanzibar

Ajali za barabarani zimeendelea kupoteza uhai wa watumiaji ambapo watu 21 walifariki kwenye ajali 28 zilizoripotiwa mwezi Disemba 2025.

Hayo yamebainishwa wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya takwimu za ajali na makosa ya barabarani kwa mwezi huo, uliofanyika Ofisi za Mtakwimu Mkuu wa serikali, Mazizini mjini Unguja jana.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtakwimu Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ahmada Hassan Suleiman, alisema, idadi ya waliofariki imeongezeka kwa asilimia 40.0 kutoka watu 15 waliofariki mwezi Novemba, 2025.

Alisema, mlinganisho wa ajali za barabarani kwa mwezi Disemba, ziliongezeka kwa asilimia 40.0 kutoka ajali 20, zilizotokea Novemba 2025.

Aidha, ajali hizo ziliacha waathirika 37 ambapo 32 walikuwa wanaume na watano wanawake huku wilaya ya Kati ikiongoza kwa waathirika 11 sawa na asilimia 29.7%, ikilinganishwa na wilaya nyengine.

“Ajali zote zilisababishwa na mwendokasi na waathirika wengi walikuwa abiria”.

Aidha, alisema, jumla ya makosa ya barabarani 9,185 yaliripotiwa mwezi Disemba ambapo 9,153 yalifanywa na wanaume na makosa 32 lilifanywa na wanawake.

Aliitaja wilaya ya Mjini ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya makosa ya barabarani 2,143 sawa na asilimia 23.3 kati ya makosa yote yalioripotiwa huku wilaya ya Micheweni ikiwa na idadi ndogo ya makosa 52, asilimia 0.6.

Alisema, idadi ya makosa iliongezeka kwa asilimia 40.7 kufikia makosa 9,185 kutoka makosa 6,528 yalioripotiwa Novemba 2025. 

Wakichangia uwasilishaji huo, baadhi ya wadau waliliomba jeshi la polisi kuendelea kupambana na madereva wanaounja sheria za usalama barabarani hasa nyakati za usiku ambazo zimeonekana ajali nyingi kutokea.

Lakini, pia aliwataka madereva kuwa makini kuepuka kusababisha ajali hasa za kuendesha mwendokasi na utumiaji wa vileo ambazo husababisha vifo au majeruhi kwa wananchi wanaotumia barabara.