NA FATMA HAMAD, PEMBA
MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed amesema endapo atapata ridhaa atawalipia deni la mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu, waliokopeshwa kwa ajili ya kusomea.
Mgombea huyo aliyasema hayo kwakati akiwahutubia wananchi ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni ulifanyika Mjimbini Mkoani mkoa wa Kusini Pemba.
Alieleza waajiriwa wengi wamekuwa wakiishi maisha duni, kutokana na mishahara yao kukatwa na kulipa deni la mikopo ya elimu ya juu.
Alisema sera ya chama chake ni kuwepo kwa elimu bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu, hivyo akiingia madarakani atawalipia madeni kwa wote ambao wanadaiwa na Bodi ya mikopo, waondokane na hali ngumu za maisha.
‘’Mishahara yenyewe midogo haikidhi haja zao halafu unakatwa, naahidi nikichaguliwa nawalipia wote wanaodaiwa, wafurahie maisha yao,’’alisema.
Aidha kwa upande mwengine alisema atawapeleka kufanya kazi nje ya nchi wafanyakazi wa kada ya uuguzi, manesi na madaktari kwenda kupata ujuzi zaidi, ili kuja kuokoa maisha ya wananchi wa Zanzibar.
Hapo awali katibu mkuu wa chama cha ADC, Mwalim Hamad Aziz alisema endapo wataingia madarakani watajenga Chuo cha Uvuvi kisiwani Pemba, ili kuzalisha wataalamu kupitia sekta hiyo.
‘’Tutakapoingia madarakani tutaanzisha chuo cha uvuvi, vijana wa Pemba wasome na kupatikana kwa wataalamu wa uvuvi na kukuza ajira kwa wingi,’’alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa kampeni wa chama hicho Hafid Khamis Amour aliwataka wananchi wa Mjimbini hususani wanawake, kukichagua chama cha ADC, ili kiwaletee maendeleo.
Aidha aliwataka wananchi hao kuwachagua viongozi ambao wanauchungu na chi yao ambao watawaletea mabadiliko majimbonimwao, na sio kuchagua kwa ajili ya chama fulani.
Hata hivyo nao baadhi ya wananchi wa Mjimbini walisema watahakikisha wanakiunga mkono chama hicho, kwani kimeonesha matumaini makubwa kwa wananchi wake.
