Skip to content

Katikakatika ya umeme kumalizika muda mfupi ujao

NA KHAMISUU ABDALLAH 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema ndani ya muda mfupi ujao Zanzibar itakuwa inajitegemea wenyewe katika nishati ya umeme, hasa kizingatiwa kuwa nishati hiyo ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Juma Malik Akil, alieleza hayo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya kimkakati ya maendeleo kwa sekta ya nishati ya umeme wa jua na upepo Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema serikali inashirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika uwekezaji wa nishati mbadala, hususan nishati ya jua, ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kupunguza utegemezi.

Alifahamisha kuwa Zanzibar hivi sasa inategemea chanzo kimoja cha nishati kinachotoka Tanzania bara na wameona sio busara kuwa na chanzo hicho tu na badala yake kutafuta vyanzo vyengine mbadala ambavyo vitawezesha wananchi wake kupata nishati hiyo kwa saa 24.

“Serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ya kiuchumi na kijamii ikiwemo maji na umeme,” alisema.

Dk. Akil alifahamisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo bandari, viwanja vya michezo, viwanja vya ndege na uwekezaji binafsi kama hoteli za kitalii, ambayo inahitaji upatikanaji wa umeme wa kutosha na uhakika.

Alibainisha kuwa uzalishaji wa megawati 400–500 utaimarisha mazingira ya uwekezaji na kuondoa changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo kwa wawekezaji.

Hivyo, aliwakaribisha wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo za hoteli, viwanda na sekta nyengine kwani serikali imejipanga kwenye hilo.

Aliipongeza serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi kwa fedha zake wenyewe bila ya kutegemea fedha za wafadhili kwa kiasi kikubwa.

“Awali utekelezaji wa miradi mikubwa ulitegemea zaidi wafadhili, lakini sasa serikali imeanza kujitegemea kwa kuwekeza rasilimali zake katika baadhi ya maeneo, hatua inayodhihirisha dhamira ya kuwahudumia wananchi na kuimarisha imani yao kwa serikali,” alisema.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, alisema huo ni muendelezo wa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili kujipanga katika mwaka mpya wa bajeti 2026/2027. 

Hivyo aliahidi ziara hiyo kuendelea kwa miradi mengine ikiwemo ya maji ili kuona inajiridhirisha na baadae kuona kiasi gani cha fedha kinaombwa katika mwaka mpya ujao wa fedha.

Dk. Juma alilipongeza Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) hasa Mkurugenzi Mkuu kwa jitihada zake anazozichukua kuhakikisha Zanzibar inapata vyanzo vya umeme na kutumia msemo usemao ‘Zanzibar bila ya ukosefu wa umeme inawezekana’.  

Naye Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Nadir Abdul-latif Alwardi, alisema serikali chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akiwapatia fedha kuhakikisha miradi ya sekta ya umeme inafanikiwa kwa lengo la kuona wananchi wanapata nishati hiyo bila ya usumbufu.

Alibainisha kuwa mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya umeme kwa kisiwa cha Pemba tayari umesainiwa na licha ya awali kukosekana kwa fedha, serikali imefanikiwa kuzipata kupitia mipango ya Wizara ya Fedha na Kamishna wa Bajeti, kwa lengo la kuhakikisha nia ya upatikanaji wa umeme wa kutosha katika kipindi kifupi kijacho.

Alipongeza Wizara ya Fedha na Mipango na timu yake kwani inawasaidia na kasi hiyo wanayokwenda nayo anaamini watamaliza miradi kwa wakati na Zanzibar ifikapo mwaka 2028 changamoto ya kuzimika umeme itaondoka.