Skip to content

Ofisi msajili wa hazina yawaonya wanaopisha ujenzi Kikwajuni

  • Blog

NA SELEMAN TAMBULEGENI

OFISI ya Msajili wa Hazina Zanzibar, imewatahadharisha wakaazi wa Kikwajuni Juu kwa Mjerumani, kuepuka kuchukua au kuharibu mali za serikali katika nyumba walizokuwa wakiishi wakati ambapo wanahama kupisha mradi wa ujenzi.

Akizungumza na Zanzibar leo, Msajili wa Hazina wa Serikali, Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, alisema onyo hilo limetokana na kuwepo kwa viashiria vya uharibifu wa miundombinu ya maji na umeme unaofanywa na baadhi ya watu katika maeneo hayo.

Alisema kumekuwepo na vitendo vya baadhi ya watu kujiamulia kuchukua mali ambazo si zao bali ni za serikali, hali inayochangia uharibifu wa mali za umma na kukiuka sheria za nchi.

Aidha, alibainisha kuwa katika nyumba ambazo zimehamwa kuna baadhi ya watu waliokuwa hawahusiki wamekuwa wakizitumia vibaya ikiwemo wizi wa vifaa vya miundombinu ya maji na umeme pamoja na wanaofanya vitendo viovu vya uasharati.

“Serikali inakusudia kuzibomoa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa nyumba za kisasa  kwa ajili ya wakaazi hawa ambao kwa asilimia kubwa wameshalipwa ili kupisha mradi na baadaye watarudi kwa utaratibu maalumu huu uharibifu unaoendelea utasababisha hasara kwa serikali, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake”, alisema Sanya.

Alisema uharibifu huo haujaishia kwenye miundombinu ya maji na umeme pekee bali pia ubomoaji wa nyumba hizo katika hali isiyozingatia utaratibu maalumu na taaluma ya uvunjaji hali inayoweza kusababisha hatari kwa majirani zao ambao bado hawajahama.

Aliongeza kuwa ili kuweka mazingira rafiki, Serikali kwa sasa imeweka askari  kulinda eneo hilo ili kuzuia vitendo hivyo, huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa mapema ili kudhibiti uhalifu.

Hata hivyo, alisema nyumba hizo zinatarajiwa kuvunjwa mwishoni mwa mwezi huu ili kuendelea na hatua nyengine za ujenzi.