SERIKALI imepanga kuwalipa fidia wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo huko Fumba Mkoa wa Mjini Magharib.
Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo Rahaleo Mjini hapa.
Alisema serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2 kwa ajili ya zoezi hilo, kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi walioathirika na miradi hiyo.
Alifafanua kuwa fidia hiyo itawanufaisha wananchi wa eneo la Dimani Dambani, ambapo jumla ya walengwa 291 wanatarajiwa kulipwa stahiki zao.
“Nawaomba wananchi wa Dimani wakae wasubiri fidia zao na wasiwe na taharuki kwani tayari tumeshafanya tathmini ya malipo yao,” alisema.
Sambamba na miradi hiyo, lakini Waziri Shariff, alisema kuna eneo kwa ajili ya ujenzi wa Goff hall lenye vishimo 18 la Kimataifa ambapo wananchi 76 watalipwa shilingi bilioni 1.28.
Pia alisema kuwa kuna eneo jengine lenye ukubwa wa heka10 ambalo wananchi wake walipisha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maendeleo.
Alisema katika eneo hilo serikali imepanga kuwekeza ujenzi wa Mji wa Michezo (AFCON) Fumba, mradi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 351.
“Mradi huu umelenga kufungua fursa za kiuchumi, kuimarisha sekta ya utalii na ajira kwa vijana”, alisema.
Pamoja na mambo mengine lakini Waziri Shariff alisema kuwa katika eneo hilo la Fumba kutajumuisha miradi kadhaa ikiwa ni pamoja na Kumbi za Mikutano ya Kimataifa ili kuongeza fursa za ukusanyaji wa mapato.
Alisema kuwa katika eneo hilo, j umla ya wananchi 242 wanatarajiwa kulipwa fidia ambapo serikali itatumia kiasi cha shilingi bilioni 1,668 kugharimu zoezi hilo.
Sambamba na hilo Waziri huyo alisema zoezi la ulipaji fidia limefanyika kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria na kuhakikisha kila mwananchi anayestahiki anapata haki yake bila ya upendeleo.
“Alisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika ili kurahisisha mchakato huo na kuepusha ucheleweshaji usio wa lazima.
Vile vile Shariff aliwahimiza wananchi kutumia vyema fedha za fidia watakazolipwa kwa kuwekeza katika shughuli za maendeleo zitakazowawezesha kujikuwamua kiuchumi.
Alibainisha kuwa serikali itaendelea kufuatilia na kusimamia miradi hiyo ili kuhakikisha inaleta manufaa yaliokusudiwa kwa jamii pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
