Skip to content

Dk. Khalid ashuhudia majaribio Bandari mpya ya Mpigaduri

NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed, amezindua majaribio ya ushushaji wa mizigo katika Bandari ya Mpigaduri ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo mkubwa wa kimkakati unaolenga kuboresha huduma za bandari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo zoezi lilofanywa na kampuni ya Azam Marine, alisema lengo ni kupunguza msongamano katika bandari ya Malindi na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji wa baharini.

Aidha alisema zoezi rasmi la ushushaji mizigo linatarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka huu baada ya kukamilika kwa majaribio hayo ya awali. 

Alisema uwepo wa bandari hiyo ya kisasa, utasaidia kuongeza ufanisi katika sekta ya uchukuzi na biashara hapa Zanzibar.

“Kukamilika kwa bandari hii mpya kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar na kuongeza ushindani wa kibiashara, kuboresha mazingira ya biashara na kuinua hadhi ya Zanzibar kama kitovu cha usafirishaji wa baharini katika Ukanda wa Afrika Mashariki”, alisema.

Hata hivyo alifahamisha kuwa bandari ya Malindi kwa sasa imezidiwa na msongamano wa abiria na mizigo hali inayosababisha ucheleweshaji wa huduma hasa kwa wafanyabiashara wanaoleta mizigo yao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, alisema bandari hiyo imejengwa na kampuni ya ZF DEVCO kwa kushirikiana na Serikali, ikiwa ni sehemu ya kuboresha miundombinu ya usafiri hapa Zanzibar.

Alisema bandari hiyo itakapomalizika kwa awamu zote itawezesha meli za mizigo kufunga saa 24 hatua itakayowezesha kuondoa foleni za meli kuja kufunga na kupata ukuta haraka.

Akif alibainisha kuwa ujenzi wa bandari hiyo ni hatua muhimu katika kukuza uchumi na kuboresha huduma za usafiri wa baharini Zanzibar.

Akizungumzia bandari ya Malindi alisema mpango mkakakati wa muda mrefu ifikapo mwaka 2028 bandari hiyo itakuwa maalum kwa ajili ya utalii.

Kwa upande wake, Meneja wa Azam Marine, Ali Mohamed, alisema bandari hiyo itasaidia kupunguza muda wa kushughulikia mizigo na kuongeza ufanisi wa kazi zao za kila siku.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake kwa jitihada za ujenzi wa bandari hiyo ambayo italeta manufaa kwa nchi na wawekezaji nchini.