Skip to content

Waziri Kitwana ataka wananchi kutoshtuka na askari wa vikosi

NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema changamoto kubwa ya baadhi ya wananchi wa Zanzibar ni kubeza na kutojikubalisha kufuata misingi na taratibu za kisheria zilizopo.

Aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha utekelezaji wa mafanikio ya siku 100 ya kipindi cha pili cha uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Rahaleo.

Alisema kuna baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia hatua za serikali kutumia vikosi vyake katika operesheni ya maeneo ya biashara kupitika kwa urahisi jambo ambalo kwa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu inakuwa kero kubwa kwa watu wengine wanaofuata bidhaa hasa eneo la Mjini Unguja maarufu Darajani.

Waziri Kitwana alisema mara nyingi watu wanashindwa kutafautisha namna ya kutii sheria bila kushurutishwa jambo ambalo mamlaka husika inapotekeleza wajibu wake hupelekea malalamiko kwa wanaovunja sheria.

“Kwa sasa vikosi viko katika operesheni ya kuona mji unakuwa salama unapitika kwa urahisi, usafiri wa umma unapatikana bila shida na sio kuwa na msongomano, biashara zinauzika na hakuna ukiukwaji wa sheria jambo ambalo linaonekana watu wengine kukereka”, alisema.

Alifahamisha kuwa lengo la serikali au wizara husika si kuwakomoa watu bali ni kufanya shughuli za kijamii kama usafiri wa umma na huduma za biashara kwa usalama na bila ya tatizo lolote kama inavyokuwa miaka ya nyuma hasa kipindi kama hichi.

Akifafanua kuhusiana na uvaaji wa ‘mask’ viziba uso, waziri Kitwana alisema uvaaji wa ‘mask’ sio tatizo na wala wanachi hawapaswi kushtuka wala kuogopa hasa kwa kuwa hakuna mtu aliepigwa wala kuumizwa kwa askari hao kutekeleza majukumu yao.

“Sisi hapa ni watu tunaojuana, muhali katika mambo kama haya huchukua nafasi yake, kuvaa huko mask au kubeba silaha kusiwashtue watu ni kutaka watu wasiwatambue askari wetu kwa urahisi, hii ni kulinda usalama wao, lakini tunawataka kutekeleza majukumu yao bila ya kudhuru watu na hicho ndicho kinachofanyika”, alisema.

Akizungumzia kuhusiana na suala la usafi, alisema vikosi sio jukumu lao kusimamia lakini wamekuwa wakifanya hivyo kwa lengo la kuimarisha huduma na kuleta haiba hasa eneo la Mji mkongwe.

Alifahamisha Waziri Kitwana pamoja na kuwepo kwa picha mitandaoni zinazorushwa ambazo zinaonesha unyanyasaji wa wananchi huku akieleza kwamba wizara inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kutambua uhalisia wa picha hizo na sheria ichukue nafasi yake.

“Tunafahamu urushwaji wa picha za matokeo ya vitendo hivi kumedhamiria kuchafua zoezi la operesheni kwani huenda picha hizo ni za matokeo ya nyuma kabisa, hata hivyo wizara itafanya uchunguzi.

Hata hivyo, Kitwana aliwataka wanajamii kuona umuhimu wa kutunza amani na usalama katika maeneo wanayoishi jambo ambalo nchi zisizo amani wanajutia hali hiyo.