Skip to content

Maabara ya Mkemia Mkuu yafungua fursa mpya za ajira kwa vijana

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

Imeelezwa kuwa utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeanza kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa vijana nchini, hususan katika sekta zinazohusiana na sayansi, mazingira na usimamizi wa kemikali.

Kupitia huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara pamoja na udhibiti wa kemikali, vijana wanapata nafasi ya kujiajiri na kukuza biashara zao kwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama wa bidhaa.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika kipindi cha Januari 2025 hadi Februari 2026.

Alisema katika kipindi hicho mamlaka imejikita katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa kimaabara, usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani, ujenzi wa miundombinu ya maabara na ofisi, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali.

“Huduma za uchunguzi wa kimaabara zinazotolewa na mamlaka zimeimarika kupitia maabara saba zilizoidhinishwa kimataifa kwa viwango vya ISO 17025:2017. Maabara hizo zinajumuisha uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, chakula, maikrobaiolojia, sayansi jinai toksikolojia, sayansi jinai kemia na mazingira ambazo zinapatikana Dar es Salaam na katika Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza,” alisema.

Aidha alieleza kuwa katika kipindi hicho mamlaka ilifanikiwa kufanya uchunguzi wa kisayansi wa jumla ya sampuli 247,286 kutoka kwa taasisi mbalimbali za serikali na wadau binafsi. Miongoni mwa taasisi zinazotumia huduma hizo ni Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na hospitali na taasisi zinazohusika na usalama mahali pa kazi na mazingira.

Aliongeza kuwa matokeo ya uchunguzi wa kimaabara yameendelea kuwa na mchango mkubwa kwa jamii kwa kusaidia kudhibiti dawa za kulevya, kuthibitisha ubora wa dawa asili pamoja na kusaidia uchunguzi wa kisayansi katika masuala ya kijamii kama uhalali wa wazazi kwa watoto na utatuzi wa migogoro ya mirathi kupitia uchunguzi wa vinasaba.

Aidha, huduma hizo zimekuwa na mchango muhimu katika sekta ya afya kwa kusaidia utambuzi wa sumu kabla na baada ya kifo pamoja na kusaidia matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum kama kusafishwa figo au kupandikizwa figo, hali inayochangia kuimarisha afya ya jamii na kuongeza uwezo wa wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Katika kuimarisha huduma hizo, mamlaka imefanikiwa kuwekeza katika mitambo mikubwa 32 ya kisasa pamoja na vifaa vidogo 542 vya uchunguzi wa kimaabara, uwekezaji uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 32.25, Uwekezaji huo umewezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma za uchunguzi wa kisayansi nchini.

Alisema kupitia huduma hizo vijana wajasiriamali sasa wanapata fursa ya kutumia maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali kupima na kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kabla ya kuziingiza sokoni ndani na nje ya nchi.

Aidha wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofanya tafiti za kisayansi wamepewa punguzo la asilimia 75 ya gharama za uchunguzi wa maabara ili kuwasaidia kukuza ujuzi na ubobezi katika maeneo ya sayansi.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria Na. 8 ya mwaka 2016. Kabla ya hapo taasisi hiyo ilikuwa wakala wa serikali ulioanzishwa kupitia Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 ikiwa sehemu ya Wizara ya Afya.