NA MWANTANGA AME
Tatizo la afya ya akili Zanzibar limeongezeka katika jamii, huku wanawake wajawazito na watoto wakitajwa kuwa miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi, hali inayohitaji juhudi za pamoja, ili kupunguza changamoto hiyo.
Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar, Dk. Salim Slim, alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya afya ya akili kwa watendaji wa Afya ya Jamii (CHWs) kutoka katika shehia mbali mbali za Mkoa wa Kusini Unguja.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani, yaliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Unguja, ambayo yalilenga kuwajengea uwezo watendaji hao, ili kusaidia jamii kukabiliana na changamoto za afya ya akili.
Dk. Slim alisema, tatizo la afya ya akili bado linaongezeka katika visiwa vya Unguja na Pemba, jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kwa haraka, ili kupunguza athari zake kwa jamii.
Alifafanua kuwa takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka takriban asilimia 1 ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 hukumbwa na changamoto za afya ya akili, huku karibu asilimia 30 ya wanawake wajawazito wakikabiliwa na matatizo hayo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara mbalimbali ikiwemo kujifungua kabla ya wakati, kupata watoto wenye mtindio wa ubongo na matatizo mengine ya kiafya.
Aidha, alisema juhudi za serikali katika kuhamasisha huduma za afya zimeanza kuzaa matunda, kwani idadi ya wanawake wanaohudhuria kliniki imeongezeka na kufikia asilimia 62,000 hatua inayosaidia kupunguza matatizo ya kiafya kwa wajawazito.
Alifahamisha kuwa awali wanawake wengi hawakuzingatia huduma za kliniki, lakini kwa sasa wengi wao wanahudhuria huduma hizo, pamoja na kuwapatia watoto wao chanjo muhimu.
Alisema katika jamii kumekuwa na wanawake wengi wanaopata matatizo katika maisha yao ikiwemo kupigwa huku wakiwa na ujauzito jambo ambalo huwasababishia kutokuwa sawa katika akili zao, lakini elimu hiyo itawasaidia kupunguza matatizo hayo katika shehia zao.
“Tusipowaunga mkono wanawake hatuwezi kutengeza taifa lililobora sisi kama serikali Wizara ya Afya nguvu kubwa yetu ni kuwekeza kwa Mama na Mtoto, Wanawake kama konde utachokitia kama kuna rutba kitaota na ikiwa hukuishughulikia unaiwacha unadai hayaoti kumbe wewe hukuishughulikia sasa wanawake na watoto ndio muhimu kwa serikali yetu” alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation, Sabra Mohamed Ali, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwafanya watendaji wa afya ya jamii kuwa mabalozi wa kuhamasisha umuhimu wa afya ya akili katika jamii.
Alisema pia kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, huku baadhi ya kesi zikiwa haziripotiwi katika vyombo husika, jambo ambalo linachangia matukio ya afya ya akili kuongezeka Zanzibar.
Mapema, Mkurugenzi wa Wanawake na Watoto katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Siti Abbas Ali, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto ya afya ya akili.
Alifafanua kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea kuongezeka, ambapo mwaka 2024 kuliripotiwa jumla ya kesi 1,809 za ukatili wa kijinsia, huku mwaka 2025 matukio hayo yakifikia 1,228.
Alisema baadhi ya waathirika wa vitendo hivyo wanahitaji msaada wa kisaikolojia, ili kurejesha hali yao ya kawaida.
Alisisitiza kuwa watendaji hao wana jukumu muhimu la kuelimisha jamii katika shehia mbalimbali, kwani serikali peke yake haiwezi kuwafikia wananchi wote katika shehia 388 zilizopo Zanzibar na kuwapa elimu hiyo.
