NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imeandika historia ya kipekee kwa kupitia tukio la futari ya kitaifa lililofanyika juzi kwa mara ya kwanza, lililowakusanya maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu pamoja.
Alhaj Dk. Mwinyi alieleza hayo alipokuwa akitoa salamu zake kwa watu waliohudhuria futari hiyo iliyofanyika Machi 7, mwaka huu katika uwanja wa New Amaan Complex, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alieleza kuwa tukio hilo ni jambo jema na lenye thawabu nyingi mbele ya Mwenyezi Mungu, sambamba na kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla katika kuimarisha mshikamano, upendo na umoja.

Aidha alizishukuru Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), kwa juhudi zao za kuandaa tukio hilo kubwa lililowakutanisha watu wengi kwa pamoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Kupitia tukio hili nawanasihi waumini wenzangu kuendelea kuzidisha ibada, dua na kufanya matendo mema katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, huku tukiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuijalia nchi amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi wake”, alieleza Dk. Mwinyi.
Kwa upande wake, Naibu Mufti wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, alisema futari hiyo ni tukio muhimu linaloongeza mapenzi na upendo miongoni mwa waumini na kuondoa chuki na kuimarisha mshikamano kati ya makundi mbalimbali ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa ZBC, Ramadhani Bukini na katibu mtendaji wa kamisheni ya utalii, akif abbas manji, walieleza kuwa wameandaa tukio hilo kama sehemu ya kuonesha umoja na mshikamano wa wananchi na viongozi wao lakini pia kuitangaza Zanzibar kimataifa kama njia ya kuvutia utalii halali.
“Tukio hili ni miongoni mwa mikakati yetu ya kuutangaza utalii wa nchi yetu tukilenga kuvunja rekodi ya dunia ambapo tunataraji watu 15,000 kufutari pamoja uwanjani hapa”. Alieleza Akif akiwashukuru wadau na tasisi mbali mbali zilizofanikisha tukio hilo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali Zanzibar (OCGS), watu 27,345 walihudhuria kwenye futari hiyo wakiwemo wanaume 18,771 sawa na asilimia 68.6 na wanawake 8,574, asilimia 31.4.

